Nov 10, 2020 16:19 UTC
  • Lissu aondoka Tanzania kuelekea Ubelgiji akisindikizwa na maafisa wa ubalozi wa Ujerumani

Tundu Antipas Lissu, aliyegombea urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28 kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ameondoka nchini humo kwenda Ubelgiji.

Lissu ameondoka nchini leo saa 11 jioni kwa ndege ya Shirika la Ndege la Ethiopia akielekea Ubelgiji ambako alikuwa akiishi kwa takribani miaka miwili kwa ajili ya matibabu.

Vyombo vya habari nchini Tanzania vimeripoti kuwa, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam (JNIA), Lissu, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), amesindikizwa na maofisa wa ubalozi wa Ujerumani, Marekani, ndugu, jamaa na marafiki.

Tundu Lissu amesema, ameamua kuondoka Tanzania, pamoja na mambo mengi, kunusuru maisha yake na "kujipanga upya kisiasa".

Akizungumza na mwandishi wa habari wa tovuti ya habari ya Mwanahalisionline Lissu amesema, haendi uhamishoni Ulaya; na au kama mkimbizi wa kisiasa; na akaongeza kuwa "nakwenda kama mtu anayerudi alikokuwa ili kujipanga upya kisiasa."

Tundu Lissu alipokuwa akipatiwa matibabu nje ya nchi baada ya kushambuliwa kwa risasi

Mbunge huyo wa zamani wa Singida Mashariki, aliyewahi pia kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) amesema "mimi si mtu wa kukimbia vita. Maisha yangu yote, nimekuwa mtu wa mapambano".

Alipoulizwa anatoa wito gani kwa wananchi waliompigia kura na Watanzania wote, Lissu amesema, "ujumbe wangu kwao, ni kwamba mimi sikimbii mapambano. Nakwenda kufungua uwanja mwingine mpya wa kudai haki, demokrasia na utu wetu kwa nchi yetu."

Hivi karibuni na baada ya kumalizika uchaguzi mkuu wa Tanzania, Tundu Lissu alisikika akisema amekuwa akitishiwa maisha yake, hali iliyomfanya yeye na wasaidizi wake kukimbilia ubalozi wa Ujerumani jijini Dar es Salaam Jumatano ya tarehe 4 Novemba ili kuomba hifadhi.

Kupatikana taarifa kwamba maisha ya mwanasiasa huyo machachari wa upinzani nchini Tanzania yako hatarini, kunakuja miaka mitatu tangu aliposhambuliwa kwa risasi na wanaoitwa "watu wasiojulikana" mchana wa tarehe 7 Septemba 2017 huko Dodoma alipokuwa akirejea nyumbani kwake kutoka bungeni alikohudhuria mkutano wa bunge.

Baada ya shambulio hilo lililomjeruhi vibaya, Lissu alisafirishwa hadi Nairobi Kenya kwa matibabu zaidi na hatimaye nchini Ubelgiji…/

 

Tags