Nov 13, 2020 01:34 UTC
  • Mazungumzo ya Tunis na makubaliano ya kuitisha uchaguzi nchini Libya

Mazungumzo baina ya pande mbalimbali za Libya yanaendelea Tunis, mji mkuu wa Tunisia kwa kusimamiwa na Umoja wa Mataifa. Lengo la mazungumzo hayo ni kuleta amani ya kudumu katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika. Taarifa za karibuni kabisa zinasema kuwa, washiriki wa mazungumzo hayo wamefikia makubaliano ya kuitisha uchaguzi nchini Libya katika kipindi kisichopindukia miezi 18 ijayo.

Rais Kais Saied wa Tunisia, Bi Stephanie Turco Williams, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya, shakhsia 75 wa kada mbalimbali za Libya pamoja na maafisa tofauti wanaohusika na mgogoro wa nchi hiyo, wanashiriki katika mkutano huo unaofanyika kwa njia ya Intaneti. Washiriki wa mkutano huo wamekubaliana kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na kuandaa miundo wa kisheria ya kuwezesha kufanyika uchaguzi wa bunge na rais nchini humo kwa usalama na utulivu.

Kikao hicho kimeitishwa baada ya pande mbili kuu hasimu za Libya kusimamisha vita baina yao mwezi Oktoba mwaka huu.

Rais Kais Saied wa Tunisia katika mazungumzo ya Libya

 

Libya imetumbukia kwenye mgogoro kwa miaka mingi. sasa hivi nchi hiyo inatawaliwa na serikali mbili hasimu, moja ya Mashariki na nyingine ya Magharibi. Kila moja ya serikali hizo ina sera na lengo la kuidhibiti nchi nzima na kuunda serikali yake moja. Serikali ya Magharibi inaongozwa na Waziri Mkuu Fayez al Sarraj na inatambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa. Makao makuu ya serikali hiyo ni Tripoli, mji mkuu wa Libya. Nyingine ni ile yenye makao yake mjini Tobruk, mashariki mwa Libya. Inaongozwa na jenerali Khalifa Haftar anayeungwa mkono na nchi kama Imarati, Misri, Saudi Arabia na Ufaransa. Serikali ya magharibi mwa Libya inaungwa mkono na nchi kama Uturuki, Qatar, Italia, Algeria na Umoja wa Ulaya. Kwa muktadha huo tutaona kuwa Libya sasa hivi imekuwa ni uwanja wa mapigano na mashindano baina ya madola ya kigeni ya ndani na nje ya bara la Afrika. Uingiliaji wa madola ya kigeni nchini Libya ni mkubwa kiasi kwamba kuna hatari hata ya kugawika vipande vipande nchi hiyo. 

Bi Stephanie Williams, mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya analalamikia sana uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya nchi hiyo na kusema, kwa hakika wananchi wa Libya wana wasiwasi na mustakbali wa nchi hayo, wamechoshwa na vita na kila mmoja wao natamani kupatikane amani ya kudumu nchini humo. 

 

Kuenea maambukizo ya kirusi cha corona, kuongezeka matatizo ya kiuchumi, vita na mapigano, hatari ya kushadidi vitendo vya magenge ya kigaidi na mambo kama hayo yameifanya jamii ya kimataifa isichoke kufanya juhudi za kuiokoa Libya licha ya kuvunjika mara kadhaa mazungumzo ya amani na kukwama juhudi mbalimbali za kuleta utulivu huko Libya. Sasa hivi juhudi hizo zimezaa matunda ya kupatikana utulivu wa kiasi fulani baada ya pande mbili kuu hasimu kufikia makubaliano ya kusimamisha vita. Inachotarajiwa ni kuona usitishaji vita huo unaendelea na juhudi za kuutatua kikamilifu mgogoro wa nchi hiyo kwa njia ya mazungumzo zinazaa matunda. Hata serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya nayo iliundwa baada ya mazungumzo yaliyosimamiwa na Umoja wa Mataifa, hivyo umoja huo unaonekana ndio unaofaa zaidi kuwa mpatanishi baina ya makundi hasimu ya Libya.

Peter Millett, balozi wa zamani wa Uingereza nchini Libya anasema: Lengo kuu la mazungumzo hayo, ni kufikiwa makubaliano kuhusu tarehe ya karibuni zaidi ya kuitisha uchaguzi. Balozi huyo anaamini kwamba suala hilo linahitajia kutolewa ujumbe wa wazi na jamii ya kimataifa kwamba yeyote atakayekwamisha juhudi hizo basi atawekewa vikwazo.

Umoja wa Mataifa umezitaka nchi zote za kigeni ziache kuingilia masuala ya ndani ya Libya. Umoja huo umezishutumu nchi hizo kutokana na kuvunja kwao marufuku ya kuyauzia silaha makundi ya Libya. Juhudi zote hivi sasa zimeelekezwa kwenye kuleta amani ya kudumu na kujenga Libya yenye utulivu na inayotawaliwa na sheria. Hata hivyo na licha ya kuweko matumaini yote hayo, lakini njia ya kufikia malengo yaliyokusudiwa ni nzito na si tambarare. Kuendelea uingiliaji wa madola ya kigeni ambayo kila moja linataka kuwa na ushawishi mkubwa zaidi nchini Libya ni miongoni mwa vikwazo vikuu vya kufikiwa malengo hayo. Nchi zilizojiingiza kwenye mgogoro wa Libya haziko tayari kufumbia macho maslahi yao ya kisiasa na kiuchumi nchini humo. Aidha kuna wasiwasi mkubwa kwamba, kioo chepesi cha amani na utulivu wa kiwango fulani uliopo Libya hivi sasa, kinaweza kuvunjwa wakati wowote kwa kurushiwa jiwe tu na maadui wa taifa hilo.

Tags