Nov 13, 2020 01:37 UTC
  • Ndege za kivita za Ethiopia zashambulia maghala ya silaha huko Tigray

Jeshi la Ethiopia limetangaza kuwa limetekeleza mashambulizi katika maghala ya silaha na kambi za kuhifadhia nishati za Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray (The Tigray People's Liberation Front (TPLF)) kaskazini mwa nchi hiyo.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ameliamuru jeshi kuwashambulia wapiganaji wa harakati ya TPLF ambao wanadhibiti eneo la Tigray kufuatia kuongezeka hitilafu kati ya serikali ya Addis Ababa na viongozi wa eneo hilo. Ndege za jeshi la Ethiopia kwa mara kadhaa zimetekeleza mashambulizi dhidi ya ngome za harakati ya TPLF. Ripoti zinasema kuwa, mamia ya wapiganaji kutoka pande mbili wameuliwa na kujeruhiwa katika mapigano baina ya jeshi la Ethiopia na wanamgambo wa Harakati ya Wananchi ya Ukomozi wa Tigray. 

Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa Ethiopia  

Kamanda wa kikosi cha Jeshi la Anga la Ethiopia ametangaza kuwa, ndege za kivita za nchi hiyo zimeshambulia maghala ya silaha na kambi za kuhifadhia mafuta za harakati ya TPLF huko Tigray.  

Tigray ni eneo la jamii ya wachache lakini wenye nguvu ambao kwa miongo kadhaa wamekuwa wakiongoza muungano tawala nchini Ethiopia.  

Muungano mpya wa utawala ulioundwa miaka miwili iliyopita baada ya kuingia madarakani Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed umesusiwa na jamii ya watu wa Tigray.

Tags