Nov 13, 2020 08:05 UTC
  • Wahajiri 74 wafariki dunia katika ajali mbaya ya baharini iliyotokea kwenye pwani ya Libya

Shirika la Kimataifa la Uhajiri (IOM) limesema, wahajiri wasiopungua 74 wamefariki dunia baada ya chombo walichosafiria kuzama katika ajali mbaya iliyotokea kwenye pwani ya Khoms nchini Libya.

Kwa mujibu wa IOM, watu zaidi ya 120 walikuwa wameabiri ndani ya chombo hicho, wakati ajali ya hiyo mbaya ilipotokea.

Taarifa ya Shirika la Kimataifa la Uhajiri imeeleza kuwa walinzi wa pwani ya Libya na wavuvi wamewaokoa watu 47 katika ajali hiyo ambayo haipungui kuwa ni ya saba kutokea katika Mediterania ya Kati tangu Oktoba Mosi mwaka huu.

Mkuu wa IOM nchini Libya Federico Soda amesema, ongezeko la roho za watu zinazopotea katika bahari ya Mediterania ni kilelezo cha jinsi nchi zinavyoshindwa kuchukua hatua za maana zinazohitajika katika utafutaji na pia kwa kukosa kuwa na uwezo wa kutosha wa uokozi katika kivuko hicho hatari zaidi cha baharini duniani.

Wahajiri wakiogelea ili kujaribu kuokoa maisha yao

Uzito wa maafa ya ajali hiyo ulidhihirika zaidi baada ya kitoto kichanga cha kiume kuaga dunia saa chache baada ya kuopolewa majini katika operesheni ya uokozi iliyohusisha meli ya kikosi cha Open Arms ambacho ndicho chombo pekee cha misaada kinachofanya kazi ya uokozi kwa sasa katika Mediterania ya Kati.

Mtoto huyo mchanga alikuwa mmoja wa manusura 111 waliookolewa siku ya Jumatano wakati mtumbwi wa mpira uliokuwa umewabeba ulipokuwa ukizama katika pwani ya Libya na ni mmoja wa watu wasiopungua 19 akiwemo mtoto mwingine mmoja waliofariki dunia katika bahari ya Mediterania katika kipindi cha siku mbili zilizopita.

Shirika la Kimataifa la Uhajiri limeripoti kuwa, watu wasiopungua 900 wameghariki na kupoteza maisha katika bahari ya Mediterania mwaka huu, baadhi yao kwa kuchelewa kuokolewa; wakati wengine zaidi ya 11,000 wamerejeshwa nchini Libya, ambako limesema si mahala salama kwao kutokana na kuishia kuwekwa kizuizini ambako kunafanyika vitendo vya ukiukaji haki za binadamu, magendo ya binadamu na utumiwaji mbaya wa watu.../

 

Tags