Nov 13, 2020 11:27 UTC
  • Nchi za Afrika zina wasiwasi kuhusu oparesheni ya Al-Shabab ya kuajiri wapiganaji Somalia

Mawaziri wa nchi za Afrika ambazo zina askari katika kikosi cha kulinda amani nchini Somalia wamebainisha wasiwasi wao kuhusu kampeni ya kundi la Al-Shabab ya kuajiri wapiganaji wapya nchini Somalia.

Mawaziri hao kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Ethiopia na Djibouti walikutana kwa njia ya video kujadili hali ya usalama nchini Somalia ambapo wametoa taarifa ya pamoja na kubainisha wasiwasi wao kuhusu tishio linaloendelea kutoka kwa kundi hilo ambalo mbali na kuwaajiri wapiganaji wapya pia linanunua silaha zaidi.

Mkutano huo ulifanyika kufuatia ripoti kuwa magaidi hao wa kundi la Al-Shabab wameanzisha kampeni ya kuajiri kwa nguvu wapiganaji wapya katika mkoa wa kusini nchini Somalia.

Kundi hilo linalodhibiti maeneo mengi ya mikoa ya kusini linaripotiwa kushinikiza viongozi wa vijiji vya mikoa hiyo kuhakikisha vijana wanajiunga na kundi hilo, hali ambayo imesababisha mamia ya vijana kukimbia maeneno hayo.

Wanajeshi wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Afrika maarufu kama AMISOM walioko Somalia ni kutoka Uganda, Kenya, Burundi, Somalia, Ethiopia na Djibouti . 

Askari wa Uganda walio katika kikosi cha kulinda amani cha AMISOM nchini Somalia

AMISOM ina askari wapatao 21,000 nchini Somalia ambao wanalinda amani katika nchi hiyo inayosumbuliwa na vita vya ndani kwa robo karne sasa.

Somalia ilitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe mwaka 1992 na katika miaka ya hivi hivi karibuni imeshuhudia kushadidi hujuma za magaidi wa al-Shabab na hivyo kuwasababishia raia wa nchi hiyo matatizo makubwa.

Askari wa AMISOM wamekuweko nchini Somalia tokea mwaka 2007 ili kujaribu kukabiliana na magaidi wa al-Shabab. Hata hivyo pamoja na jitihada hizo za kimataifa, magaidi wa al-Shabab wanaendelea kutekeleza hujuma Somalia na nchi jirani ya Kenya.

Tags