Nov 13, 2020 11:33 UTC
  • Surua yaua watu 200,000 duniani, DRC, CAR, Madagascar zaongoza Afrika

Ugonjwa wa surua ulisababisha vifo vya watu wapatao 207,000 mwaka jana pekee baada ya muongo mzima wa mkwamo wa kupanua wigo wa utoaji chanjo, limesema shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO.

WHO imesema “idadi ya vifo mwaka 2019 ilikuwa asilimia 50 zaidi ya kiwango cha chini zaidi cha mwaka 2016 na katika kanda zote za WHO, idadi ya wagonjwa iliongezeka na kuwa wagonjwa 869,770 duniani kote.”

Mwaka huu kumekuwepo na idadi ndogo ya wagonjwa, lakini janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 linarudisha nyuma mafanikio katika utoaji chanjo, ambapo watu zaidi ya milioni 94 wako hatarini kukosa chanjo ya surua katika nchi 26 kutokana na kusitishwa kwa kampeni za chanjo, zikiwemo nchi ambazo bado zina mlipuko wa maradhi hayo.

Surua ni ugonjwa ambao unaweza kuzuilika, lakini mafanikio yake yanahitaji asilimia 95 ya watoto wote wapatiwe chanjo kwa wakati, na chanjo hiyo ni dozi mbili dhidi ya surua ambazo ni  MCV1 na MCV2. Kwa sasa utoaji wa chanjo ya surua, MCV1 imekwama duniani kote kwa zaidi ya muongo mmoja na kiwango cha utoaji ni kati ya asilimia 84 na 85, ilhali utoaji wa chanjo dhidi ya surua, MCV2 umekuwa ukiongezeka lakini kwa asilimia 71 pekee.

Mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya surua huko kambini Beerta Muuri mjini Baidoa nchini Somalia

Wiki iliyopita, UNICEF na WHO zilitoa wito wa pamoja wa kuepusha milipuko ya surua na polio, zikitaka nyongeza ya dola milioni 255 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo ili kushughulikia pengo la ukosefu wa kinga dhidi ya surua katika mataifa 45 yaliyo hatarini zaidi kupata milipuko.

Mataifa ambayo hivi karibuni yamekumbwa na milipuko mikubwa ya surua ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Madagascar, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), Georgia, Kazakhstan, Macedonia Kaskazini, Samoa, Tonga na Ukraine.

Tags