Nov 14, 2020 12:12 UTC
  • Libya: Sera za Umoja wa Ulaya zinawasukuma Waafrika upande wa kifo

Kamati ya Taifa ya Haki za Binadamu nchini Libya imekosoa vikali sera za uhajiri za Umoja wa Ulaya na kueleza kwamba, sera hizo zimekuwa zikiwasukuma Waafrika upande wa kifo.

Taarifa ya kamati hiyo imetolewa baada ya kuripotiwa habari ya vifo vya wahajiri wengine 100 waliokufa maji katika pwani ya Libya kufuatia boti zao walizokuwa wakisafiria kuzama.

Kamati ya Taifa ya Haki za Binadamu nchini Libya imesisitiza katika taarifa yake kwamba, sera mbaya za uhajiri za Umoja wa Ulaya kila siku zimekuwa zikipelekea raia wa Kiafrika kuelekea upande wa kifo.

Wahajiri wasiopungua 100 walizama na kufa maji jana Ijumaa katika pwani ya Libya katika matukio mawili ya kuzama boti walizokuwa wakisafiria.

Shirika la Kimataifa la Uhajiri (IOM) limetangaza kuwa, wahajiri wasiopungua 100 wamefariki dunia baada ya vyombo vyao viwili walivyokuwa wakisafiria kuzama katika ajali mbaya iliyotokea kwenye pwani ya Khoms nchini Libya.

Maelfu ya wahajiri aghalabu yao wakiwa ni Waafrika hufa maji kila mwaka katika ajali za majini, wakiwa na azma ya kuelekea Ulaya kusaka maisha mazuri

 

Takwimu za Shirika la Kimataifa la Uhamiaji zinaonyesha kuwa, maelfu ya wahajiri aghalabu yao wakiwa ni raia wa Afrika hufa maji kila mwaka katika ajali hizo za majini, wakiwa na azma ya kuelekea Ulaya kusaka maisha mazuri.

Mgogoro mkubwa wa wahajiri unaozizonga nchi za Ulaya umesababishwa na sera mbaya za nchi za Magharibi katika maeneo mbalimbali ya dunia hususan Asia Magharibi na vilevile umaskini mkubwa na ukosefu wa usalama katika baadhi ya nchi za Afrika.

Tags