Nov 21, 2020 02:44 UTC
  • Burundi yataka kufungwa ofisi ya mjumbe maalumu wa UN nchini humo

Serikali ya Burundi imesema haikaribishi tena kuwepo na Ofisi ya Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, na kwamba taifa hilo lina amani baada ya kushuhudia mgogoro wa kisiasa kwa miaka kadhaa.

Katika barua yake kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Albert Shingiro, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi amesema: Baada ya mchakato wa uchaguzi uliofanikiwa, na uliopelekea kushuhudiwa kipindi cha kihistoria cha mpito chenye amani na cha kupigiwa mfano barani Afrika, serikali ya Burundi inaona kuwa, uwepo wa ofisi hiyo ya UN nchini humo hauna maana tena.

Barua hiyo imeeleza bayana kuwa, ofisi hiyo ya mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa imeifanya Burundi iwe katika mzunguko wa mgogoro wa kubuniwa, unaondeshwa na watu fulani wa nchi ajinabi.

Albert Shingiro, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi amebainisha katika barua hiyo kwa Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa UN kuwa, nchi hiyo ya Afrika Mashariki imefanikiwa kupata amani, usalama na uthabiti na kwa msingi huo, haioni haja ya kuendelea kuwepo nchini  Ofisi ya Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa iliyoasisiwa mwaka 2016.

Machafuko Burundi

Ofisi hiyo iliundwa baada ya nchi hiyo kushuhudia mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na hatua ya aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Pierre Nkurunziza kutangaza kuwa atagombea muhula mwingine tata wa urais.

Hii ni katika hali ambayo,  hivi karibuni serikali ya Burundi ilitangaza kuwa, inataka kurejesha uhusiano wake na Umoja wa Mataifa ambao ulizorota katika kipindi cha utawala wa Nkurunziza, ambaye aliaga dunia mapema mwaka huu, baada ya taifa hilo kufanya uchaguzi ambao Nkurunziza mwenyewe hakugombea.

 

Tags