Nov 22, 2020 06:40 UTC
  • Uchaguzi wa Burkina Faso unafanyika leo chini ya wingu zito la ukosefu wa amani

Uchaguzi wa rais nchini Burkina Faso unafanyika leo Jumapili, Novemba 22, 2020 huku ukosefu wa amani na usalama ukiigubika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Shirika la habari la Ufaransa limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, inaonekana kwamba rais wa hivi sasa wa Burkina Faso,  Roch Marc Christian Kaboré ana nafasi kubwa zaidi ya kushinda katika uchaguzi huo wa leo.

Uchaguzi huo unafanyika huku makundi yenye silaha yakiendelea kuhatarisha usalama wa nchi hiyo ambayo ni miongoni mwa nchi maskini zaidi duniani.

Watu milioni 6 na laki tano wametimiza masharti ya kupiga kura nchini Burkina Faso. Rais wa hivi sasa,  Roch Marc Christian Kaboré anachuana na wagombea 12 katika kinyang'anyiro hicho. Kipindi cha kwanza cha urais wa Kaboré kilianza mwaka 2015.

Uchaguzi unafanyika leo Burkina Faso chini ya wingu la ukosefu mkubwa wa usalama

Maafisa wa kulinda usalama wamemiminwa katika kona zote za Burkina Faso kutokana na kuweko wasiwasi wa mashambulio ya wanamgambo wenye silaha.

Hivi karibuni wanajeshi 14 wa Burkina Faso waliuawa kaskazini mwa nchi hiyo ikiwa ni idadi kubwa zaidi ya wanajeshi kuuawa nchini humo tangu mwaka 2015.

Mashambulio ya magenge yenye silaha yanafanyika takriban kila siku huko Burkina Faso na kupelekea udhibiti wa usalama kutoka mikononi mwa serikali katika maeneo mengi ya nchi hiyo.

Katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, zaidi ya watu milioni moja wamekuwa wakimbizi kutokana na mashambulio hayo ya mara kwa mara ya magenge yenye silaha. Hiyo ni sawa na asilimia 5 ya wananchi wote wa Burkina Faso.

Tags