Nov 22, 2020 12:35 UTC
  • Jeshi la Ethiopia latoa onyo la kushadidisha mashambulio ili kudhibiti makao makuu ya eneo la Tigray

Jeshi la Ethiopia limeonya kuwa litashadidisha mashambulio yake dhidi ya Tigray ili kudhibiti makao makuu ya eneo hilo.

Kufuatia kupamba moto mapigano kati ya jeshi la serikali kuu ya Ethiopia na vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray, jeshi la serikali limeonya kuwa litatumia vifaru na mizinga ili kuyazingira na kuyadhibiti makao makuu ya eneo la Tigray.

Taarifa iliyotolewa na jeshi la Ethiopia imeeleza kuwa, awamu inayofuatia itakuwa sehemu muhimu sana ya operesheni yake ya mashambulio, ambayo itajumuisha operesheni ya kuzingira makao makuu ya Tigray kwa kutumia vifaru na kuhitimisha mapigano katika maeneo ya milimani na kusonga mbele kuelekea maeneo ya visima vya mafuta.

Mnamo tarehe 4 Novemba na baada ya kuvituhumu vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray kwamba vimewashambulia askari wa jeshi la serikali, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alitoa amri ya kushambuliwa kijeshi eneo hilo la Tigray.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed

Tigray ni eneo la jamii ya wachache lakini wenye nguvu ambao kwa miongo kadhaa wamekuwa wakiongoza muungano tawala nchini Ethiopia. 

Waziri Mkuu wa Ethiopia anafanya juhudi za kuhakikisha anaubadilisha muungano tawala katika sura ya chama kimoja, hatua ambayo imekabiliwa na upinzani wa jamii ya Watigray ambao wamekataa kushiriki katika serikali ya muungano tawala.../ 

Tags