Nov 23, 2020 03:43 UTC
  • Serikali ya Ethiopia yatoa muhula wa mwisho kwa viongozi wa Tigray kusalimu amri

Waziri Mkuu wa Ethiopia ametoa muhula wa mwisho kwa viongozi wa eneo la Tigray lililoko kaskazini mwa nchi hiyo kusalimu amri.

Abiy Ahmed ametangaza usiku wa kuamkia leo kuwa, anatoa muda wa saa 72 kwa viongozi wa eneo la Tigray kusalimu amri, vyenginevyo yataanzishwa mashambulio dhidi ya eneo hilo.

Saa kadhaa kabla ya kutolewa muhula huo wa mwisho na Abiy Ahmed, jeshi la Ethiopia lilitangaza kuwa limekusudia kuuzingira mji wa Mek'ele makao makuu ya eneo hilo la Tigray.

Mnamo tarehe 4 Novemba na baada ya kuvituhumu vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray kwamba vimewashambulia askari wa jeshi la serikali, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alitoa amri ya kushambuliwa kijeshi eneo hilo la Tigray.

Kwa kutoa amri hiyo ya kushambuliwa vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray, Waziri Mkuu wa Ethiopia alijiingiza kwenye vita ambavyo yumkini vikapelekea nchi hiyo kugawanyika.

Kifaru cha jeshi la Ethiopia

Umoja wa Mataifa umetoa indhari kuhusu taathira hasi za kuendelea vita kati ya jeshi la Ethiopia na Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray na kutangaza pia kwamba katika siku za karibuni zaidi ya watu elfu ishirini wamekimbilia nchi jirani ya Sudan ili kujinusuru na maafa ya vita hivyo na kwamba idadi ya wakimbizi hao wa Ethiopia inazidi kuongezeka.

Tigray ni eneo la jamii ya wachache lakini wenye nguvu ambao kwa miongo kadhaa wamekuwa wakiongoza muungano tawala nchini Ethiopia. 

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ambaye aliingia madarakani miaka miwili iliyopita ameanzisha muungano mpya ambao jamii ya eneo la Tigray imekataa kujiunga nao.

Abiy Ahmed anafanya juhudi za kuhakikisha anaubadilisha muungano huo tawala katika sura ya chama kimoja, hatua ambayo inapingwa na jamii ya Watigray.../