Nov 23, 2020 12:33 UTC
  • Kuendelea mgogoro wa Tigray nchini Ethiopia na hatari zake

Mgogoro katika jimbo la Tigray nchini Ethiopia umechukua muelekeo mpya ambapo Abiy Ahmed, Waziri Mkuu wa nchi hiyo amewapa viongozi wa jimbo hilo muda wa masaa 72 wawe wamejisalimisha na kuweka chini silaha zao, la sivyo, atazingira na kuyashambulia makao makuu ya eneo hilo.

Mgogoro wa Ethiopia umeongezeka na kuchukua sura mpya katika wiki chache zilizopita. Abiy Ahmed Waziri Mkuu wa Ethiopia amewatuhumu wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray TPLF kuwa waliwashambulia wanajeshi wa nchi hiyo na hivyo kutoa amri ya kushambuliwa eneo hilo la kaskazini mwa nchi, jambo limeanzisha vita vya maoja kwa moja kati ya pande mbili.

Watu wa Tigray ni jamii ya wachache na wanaunda asilimia 6 tu ya watu wote wa nchi hiyo. Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray ambayo inawakislisha watu wa eneo la Tigray kwa muda wa miaka 30 ilikuwa katika kilele cha uongozi wa Ethiopia ambapo iliiongoza nchi bila kuyashirikisha makabila mengine ya nchi hiyo. Lakini mambo yaligeuka mwaka 2018 ambapo Ahmed Abiy kutoka kabila la Oromo, ambalo ni moja ya makabila makubwa ya Ethiopia, alichukua uwaziri mkuu wa nchi.

Baada ya kuchukua hatamu za uongozi, Abiy Ahmed aliuunganisha muungano tawala wa vyama kadhaa katika chama kimoja na kukataa kuiunganisha Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray, ambayo nayo kwa miaka mingi  ilikuwa mwanachama wa muungano huo tawala katika chama hicho kipya. Watu wa Tigray wanadai kwamba serikali kuu ya Ethiopia imewapuuza na wala haizingatii maslahi yao, na hiyo ndiyo sababu ya kuongezeka hisia za kutaka kujitenga na kujitawala eneo hilo.

Waziri Mkuu Abiy Ahmed wa Ethiopia

Kabla ya matukio yanayoendelea hivi sasa huko Ethiopia, nchi hiyo ambayo ina zaidi ya watu milioni 100 na hivyo kuhesabiwa kuwa moja ya nchi za Kiafrika zilizo na idadi kubwa zaidi ya watu, imekuwa ikichukuliwa kuwa mfano bora wa kuigwa na nchi nyingine katika suala zima la kurejea kwenye mkondo wa demokrasia. Pamoja na hayo, tokea tarehe 4 mwezi huu wa Novemba, mivutano na mapigano yamezuka kati ya serikali kuu iliyo na makao yake mjini Addis Ababa na wapiganaji wa ukombozi wa Tigray, mapigano ambayo yamelazimisha maelfu ya watu wa jimbo hilo kukimbilia usalama wao katika nchi jirani ya Sudan.

Jeshi la Ethiopia limetoa taarifa likitangaza kuwa siku chache zijazo zitakuwa muhimu sana kwake kwani ndizo zitakazoainisha operesheni ya kuzingirwa Mekelle, ambayo ni makao makuu ya Tigray kwa kutumiwa vifaru na wakati huo huo kumalizwa vita katika maeneo ya milimani, suala ambalo litaruhusu kufikiwa kirahisi maeneo yenye mafuta yaliyo karibu na milima hiyo.

Kwa sasa hali ya mambo huko Tigray ni tata na yenye mgogoro mkubwa. Maelfu ya wakazi wa eneo hilo wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na madawa na wengi wao wanakimbilia usalama wao katika nchi jirani.

Babar Baloch, Msemaji wa Kamisheni Kuu ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia Masuala ya Wakimbizi anasema kwa sasa taasisi hiyo inapanga mipango ya kushughulikia mahitaji ya wakimbizi wa vita vya Ethiopia wapatao laki mbili kwa kipindi cha miezi sita ijayo.

Wapiganaji wa TPLF

Ni wazi kuwa kufikia sasa juhudi za kimataifa kwa ajili ya kutatua mzozo huo hazijafanikiwa. Abiy Ahmed amekataa kabisa juhudi zozote za kusitisha vita au hata kukubali upatanishi kwa ajili ya kutatua mgogoro uliopo.

Kwa sasa, Ethiopia inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa vita vya ndani ambao kwa upande mmoja unachochewa na uhasama wa kikabila na kwa upande wa pili unatokana na uingiliaji wa kigeni. Ethiopia ni nchi muhimu iliyo na nafasi ya kistartijia barani Afrika, hivyo kutokea vita katika nchi hiyo kunaweza kuhatarisha usalama wa eneo zima. Ni wazi kuwa vita na machafuko kama hayo yanatoa fursa kwa baadhi ya nchi zilizo na mvutano na Ethiopia kuhusiana na ujenzi wa Bwawa la Renaissance au kwa jina jingine an-Nahdha, kufuatilia malengo yao katika uwanja huo.

Kwa vyovyote vile, kuzuka vita vikubwa vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ethiopia si kwa maslahi ya yeyote yule kwa sababu vitahatarisha usalama wa eneo zima la kistratijia la kaskazini mashariki mwa Afrika na wakati huo huo kupelekea nchi hiyo muhimu kugawanyika katika sehemu ndogondogo za utawala na hatimaye kupotea umoja wa ardhi ya nchi hiyo.

Tags