Nov 24, 2020 07:23 UTC
  • Polisi ya Uganda yasema, waliopoteza maisha katika machafuko ya uchaguzi ni watu 45

Takwimu mpya zilizotolewa na jeshi la polisi nchini Uganda zinaonesha kuwa, watu waliofariki dunia katika maandamano ya fujo yaliyoikumba nchi hiyo wiki iliyopita, imepanda na kufikia watu 45.

Msemaji wa jeshi la polisi Fred Enanga amethibitisha hayo mbele ya waandishi wa habari na kutoa ufafanuzi kwa kusema, waliokufa ni wanaume 39 na wanawake sita.

Chombo kimoja cha habari nchini Uganda kimevinukuu vyanzo vya usalama vikisema kuwa ufyatuaji mkubwa wa risasi ulifanywa na watu ambao hawakuwa wamevaa sare, ambao walirekodiwa na umma wakinadi bunduki kwenye mitaa.

Maandamano yalizuka nchini Uganda baada ya jeshi la polisi kumtia mbaroni kiongozi wao Robert Kyagulanyi maarufu kwa jina la Bobi Wine wakishinikiza aachiliwe huru.

Bobi Wine alipotiwa mbaroni na jeshi la polisi nchini Uganda

 

Siku ya Ijumaa, waziri wa usalama wa Uganda, Jenerali Elly Tumwiine aliwaambia waandishi wa habari kuwa polisi na vikosi vingine vya usalama vina haki ya kufyatua risasi na kuua. 

Kabla ya ripoti hiyo ya jeshi la polisi la Uganda, ripoti nyingine zilikuwa zimesema kwamba, watu wasiopungua 68 wameuawa katika maandamano yaliyoambatana na vurugu ambayo yalianza Jumatano mjini Kampala mara tu mwanasiasa kijana Bobi Wine kutiwa mbaroni na vyombo vya usalama akiwa katika kampeni zakke za uchaguzi. Wakati huo takwimu za polisi zilisema ni watu 28 ndio waliouawa katika machafuko hayo.

Hivi sasa jeshi hilo limeongeza idadi ya watu waliouawa na kuifikisha kwenye watu 45, wanaume 39 na wanawake 6.