Nov 24, 2020 13:50 UTC
  • Kiongozi wa waasi DRC ahukumiwa kifungo cha maisha jela kwa uhalifu dhidi ya binadamu

Ntabo Ntaberi Sheka aliyekuwa kiongozi wa wanamgambo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu ukiwemo ubakaji wa watu wengi.

Mahakama ya kijeshi ilimpata Ntabo Ntaberi na hatia ya mauaji, ubakaji, utumwa wa kingono na kuwasajili watoto walio chini ya miaka 15 katika jeshi lake na kuwatumia kama askari vitani.

Uamuzi huo ulitolewa baada ya kusikilizwa kwa kesi hiyo iliyochukua takriban miaka miwili ambapo waathiriwa 178 walitoa ushahidi wao.

Umoja wa Mataifa unasema kwamba uamuzi huo umeonesha 'uzoefu wa kutenda uhalifu bila kujali una kikomo chake'.

'Uamuzi huo unawapatia matumaini waathiriwa wa mzozo huo wa DRC kwamba, mateso waliopitia yamesikilizwa na kutambuliwa', alisema Leila Zerrougui, Mkuu wa ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa uliopo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Leila Zerrougui, Mkuu wa ujumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa uliopo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo

Ntaberi anayejulikana kama Sheka, alikuwa mmoja wa viongozi wa kundi moja la wapiganaji kwa jina Nduma of Congo (NDC) ambalo lilifanya operesheni zake katika mkoa wa mashariki wa Kivu.

Eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limekuwa likishuhudia machafuko ya mara kwa mara baina ya makundi ya wanamgambo kwa upande mmoja na wanamgambo na maafisa usalama kwa upande mwingine, kutokana na kuwa na utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu na almasi. 

Wananchi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hasa wa mashariki mwa nchi hiyo wamekuwa wakilalamikia utendaji mbovu wa askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa MONUSCO na hata kuandamana wakitaka kuondoka askari hao katika nchi yao.