Nov 24, 2020 13:50 UTC
  • Viongozi wa kisiasa Algeria wakasirishwa na uingiliaji wa Macron katika masuala ya nchi yao

Matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa kuhusiana na hali ya ndani ya Algeria yamekosolewa vikali na vyama na makundi mbalimbali ya kisiasa ya nchi hiyo

Kauli ya Macron ya kuingilia masuala ya ndani ya Algeria, tamko lake la kumuunga mkono rais wa nchi hiyo na kukwepa serikali yake kuomba radhi kuhusiana na ukatili uliofanywa na Ufaransa katika kipindi ilipoikoloni Algeria vimekabiliwa na wimbi kubwa la ghadhabu na malalamiko ya vyama, viongozi wa kisiasa na vyombo vya habari vya nchi hiyo.

Katika mahojiano aliyofanyiwa wiki iliyopita, rais wa Ufaransa alimtaja rais Abdelmadjid Tebboune wa Algeria ambaye alisafiri kuelekea Ujerumani kwa ajili ya matibabu baada ya kupatwa na virusi vya corona, kuwa ni mtu shujaa; na akaahidi kufanya kila awezalo kumsaidia katika uongozi wake wa kipindi cha mpito nchini Algeria.

Karim Tabo, kiongozi wa chama kipya cha Umoja wa Kidemokrasia, na mmoja wa shakhsia mashuhuri wa harakati ya wananchi wa Algeria amesema, matamshi aliyotoa rais wa Ufaransa ni uingiliaji wa moja kwa moja katika mivutano ya ndani ya Algeria, ambao utakwamisha mchakato wa mageuzi ya kidemokrasia wa kuwawezesha wananchi kujipatia haki zao katika nchi yao.

Abdurazak Muqri

Abdurazak Muqri, kiongozi wa harakati ya Jamii ya Amani, tawi la Ikhwanul Muslimn nchini Algeria, Muhnad Uomar, Katibu Mkuu wa harakati ya “Jumuiya ya Mujahidina” na Hassan Bel Abbas kiongozi wa chama cha Muungano kwa ajili ya Utamaduni na Demokrasia wametoa kauli za kukosoa matamshi ya karibuni ya rais Emmanuel Macron wa Ufaransa na wakamtaka aache kuingilia mara kwa mara masuala ya utawala ya nchi za Afrika.

Mbali na shakhsia wa kisiasa, baadhi ya vyombo vya habari vya Algeria pia vimekosoa matamshi ya karibuni yaliyotolewa na rais wa Ufaransa…/

 

Tags