Nov 24, 2020 14:07 UTC
  • Wapiganaji wa Tigray waanza kujisalimisha; kiongozi wao aapa kutorudi nyuma

Idadi kubwa ya wapinganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray wanaripotiwa kuanza kujisalimisha kwa vikosi vya serikali ya Ethiopia masaa kadhaa kabla ya kumalizika muhula wa masaa 72 uliokuwa umetolewa na Waziri Mkuu Abi Ahmed.

Hata hivyo kumekuweko na taarifa kwamba, kiongozi wa Tigray Debretsion Gebremichael ameapa kuendelea na mapigano dhidi ya vikosi vya serikali kuu ya Addis Ababa na kupuuzilia mbali muhula wa kujisalimisha uliotolewa hivi karibuni na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed.

Siku ya Jumapili Waziri Mkuu wa Ethiopia Abby Ahmed, alitangaza makataa ya saa 72 kwa vikosi vinavyoongoza mapigano Kaskazini mwa eneo lenye utata la Tigray, kujisalimisha kwa serikali.

"Waziri Mkuu haelewi sisi ni akina nani. Ni watu na misimamo yetu na tuko tayari kufariki dunia tukitetea haki ya kujitawala eneo letu", Shirika la habari la AFP limemnukuu Bw. Debretsion, kiongozi wa chama cha Tigray People's Liberation Front (TPLF) akitoa msimamo huo.

Debretsion Gebremichael amekanusha vikali madai ya serikali ya Ethiopia kwamba mji mkuu wa eneo hilo  waMekelle umezingirwa na vikosi vya serikali.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

 

Mamia wanasemekana kuuawa huku makumi ya maelefu ya watu wakitoroka eneo hilo kwa karibu wiki tatu za mapigano.

Mnamo tarehe 4 Novemba na baada ya kuvituhumu vikosi vya Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray kwamba vimewashambulia askari wa jeshi la serikali, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alitoa amri ya kushambuliwa kijeshi eneo hilo la Tigray.

Tigray ni eneo la jamii ya wachache lakini wenye nguvu ambao kwa miongo kadhaa wamekuwa wakiongoza muungano tawala nchini Ethiopia.