Nov 25, 2020 08:12 UTC
  • Vyombo binafsi vya habari Uganda vyakataa kurusha hotuba ya Rais Museveni

Muungano wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini Uganda umekataa kurusha hewani hotuba ya Rais Yoweri Museveni wa nchi hiyo ukisisitiza kwamba kufanya hivyo ni kutoa upendeleo kwa mgombea mmoja dhidi ya wengine katika wakati huu wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Rais Yoweri Museveni alikuwa ameviagiza vyombo vyote vya habari nchini Uganda kurusha hotuba yake kila Jumapili saa moja hadi saa tatu usiku, lakini Muungano wa Wamiliki wa Vyombo Binafsi vya Habari umekataa kutekeleza agizo hilo.

Katika tamko lake, Muungano huo umesema, katika msimu wa kampeni hawawezi kutoa fursa kwa mgombea mmoja pekee bila kuzingatia wagombea wengine.

Kulingana na Sheria ya Utangazaji ya Uganda ya mwaka 2013, kila mgombea anastahili kupewa nafasi sawa katika Vipindi na Habari zinazochapishwa au kupeperushwa na vyombo vyote vya habari nchini humo.

Msemaji wa Rais Museveni, Don Wanyama, alitangaza kuahirishwa hotuba ya rais huyo wa Uganda Jumapili usiku baada ya vyombo vya habari kukataa kurusha hotuba hiyo.

Hayo yanajiri wakati kampeni za uchaguzi mkuu wa Uganda uliopangwa kufanyika tarehe 14 Januari 2021 zimeshuhudia machafuko makubwa ya umwagaji damu yaliyopelekea makumi ya watu kuuawa.

Bobi Wine baada ya kutiwa nguvuni na polisi

Watu wasiopungua 68 wameripotiwa kuuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika maandamano yaliyoambatana na vurugu ambayo yalianza Jumatano ya wiki iliyopita katika jiji kuu la Kampala mara tu mgombea urais kwa tiketi ya chama cha upinzani cha Umoja wa Kitaifa NUP, Robert Kyagulanyi maarufu kama Bobi Wine anayeonekana kuwa mwiba kwa Rais Yoweri Museveni kutiwa mbaroni na vyombo vya usalama akiwa katika kampeni zake za uchaguzi.

Asasi mbalimbali za kiraia nchini Uganda zimeonyesha wasiwasi zilionao na kueleza kwamba, machafuko hayo na jinsi vikosi vya usalama vilivyoyakandamiza maandamano ya wapinzani ni mambo yanayotilia shaka kama kweli uchaguzi ujao utafanyika katika mazingira huru na ya haki.../

 

 

Tags