Nov 25, 2020 12:18 UTC
  • Waziri Mkuu wa Ethiopia aitaka jamii ya kimataifa kujiweka mbali na mgogoro wa Tigray

Waziri Mkuu wa Ethiopia ameitaka jamii ya kimataifa kujiweka mbali na mgogoro unaoendelea wa jimbo la Tigray lililoko kaskazini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.

Abiy Ahmed amesema hayo baada ya kutolewa wito wa kusitishwa vita huko Tigray ambapo amesisitiza kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kujitenga mbali na uingiliaji wowote ule usio wa kisheria na usiokubalikaWaziri Mkuu wa Ethiopia ameitaja operesheni ya jeshi la nchi hiyo huuko Tigray kuwa ni ya 'kuokoa sheria'.

Akizungumza mapema leo, Abiy Ahmed amesema, linapokuja suala la msaada, jamii ya kimataifa inapaswa kukaa kando kwanza mpaka serikali ya Ethiopia itakapowasilisha ombi la kutaka kusaidiwa.

Jana Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliakhirisha kujadili kadhia ya mgogoro wa Tigray baada ya mataifa ya Afrika kutaka zipatiwe muda zaidi juhudi za kidiplomasia zinazofanywa na Umoja wa Afrika kwa ajili ya kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.

Debretsion Gebremichael, Kiongozi wa Tigray

 

Hayo yanajiri katika hali ambayo, watu 700 wametiwa mbaroni nchini Ethiopia sambamba na kushadidi mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo na wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Wananchi wa Tigray.

Raia hao wametiwa mbaroni kwa tuhuma za kufanya maandamano dhidi ya serikali na kujihusisha na vitendo vya utumiaji mabavu katika mji mkuu wa nchi hiyo Addis Ababa.

Katika upande mwingine, muhula wa saa 72 uliokuwa umetolewa na Waziri Mkuu wa Ethiopia kwa viongozi wa eneo la Tigray kusalimu amri, vyenginevyo yataanzishwa mashambulio dhidi ya eneo hilo unamalizika leo.

Tags