Nov 26, 2020 08:10 UTC
  • Watu 12 wauawa katika mashambulio mawili ya kigaidi huko Somalia

Maafisa usalama wa Somalia wametangaza kuwa, watu 12 wameaga dunia katika mashambulio mawili tofauti ya kigaidi nchini humo.

Maafisa hao wameripoti kuwa, askari polisi wasiopungua watano wa Somalia wamepoteza maisha na wengine wawili kujeruhiwa katika mlipuko wa bomu la kutegwa ardhini uliotokea katika barabara inayoelekea Mogadishu mji mkuu wa nchi hiyo. Hadi sasa hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo ya kigaidi hata hivyo mshambulizi kama hayo huko Somalia aghalabu hufanywa na kundi la kigaidi la al Shabaab.  

Magaidi wa kundi la al Shabaab  

Wanachama wa kundi la kigaidi la al Shabaab aidha wameishambulia nyumba ya mkazi mmoja wa Kisomali katika mji wa Wajid huko Bakol kusini magharibi mwa Somalia na kuwaua watu saba wa familia hiyo.  

Maafisa usalama wa Somalia wamesema kuwa, mwanajeshi mmoja wa jeshi la Somalia alikuwa akiishi na familia yake kwenye nyumba hiyo ambayo imeshambuliwa na magaidi wa al Shabaab. Kufuatia hujuma hiyo ya magaidi wa al Shabaab, mwanajeshi huyo na wenzake sita wa familia hiyo wakiwemo watoto wadogo watatu walio na umri chini ya miaka mitano wameuliwa katika uvamizi huo.  

 Al Shabaab ni kundi la kigaidi ambalo lilitangaza uwepo wake huko Somalia tangu mwanzoni mwaka 2004; kundi ambalo lina fikra na aidiolojia zenye mfungamano na za mtandao wa kigaidi wa al Qaida. 

Tags