Nov 26, 2020 09:44 UTC
  • Kuendelea malalamiko ya Wanigeria katika kumtetea Sheikh Zakzaki

Katika kuendelea kushikiliwa kinyume cha sheria Sheikh Ibrahim Zakzaki, Kiongozi wa Waislamu wa Nigeria, Waislamu wa nchi hiyo kwa mara nyingine tena wamefanya maandamano makubwa ya kuunga mkono na kutaka mwanzuoni huyo wa Kiislamu aachiliwe mara moja.

Waandamanaji waliokuwa wamebeba maberamu yaliyokuwa na picha na maandishi ya kumuunga mkono mwanazuoni huyo katika maandamano hayo yaliyofanyika Abuja, mji mkuu wa Nigeria, walipiga nara za kutaka achiliwe huru mara moja kwa kutilia maanani kwamba anaendelea kuzuiliwa kinyume cha sheria za nchi hiyo.

Sheikh Zakzaki alitiwa nguvuni akiwa na mke wake mnamo tarehe 13 Disemba 2015 kufuatia shambulio lililofanywa na wanajeshi wa Nigeria kwenye huseiniya yake katika mji wa Zaria. Ni miaka mitano sasa tokea wakamatwe, na mashinikizo ya wanajeshi dhidi ya Waislamu wa nchi hiyo yanaendelea kuongezeka kila siku. Lakini licha ya mashinikizo hayo yote, Waislamu wamekuwa wakiyastahamili na kuendelea kufanya maandamano katika miji tofauti ya Nigeria wakitaka kiongozi wao aachiliwe bila masharti yoyote. Mengi ya maandamano hayo yamekuwa yakivunjwa kwa mkono wa chuma wa jeshi na askari usalama.

Sheikh Zakzaki akiwa na mke wake kizuizini

Hii ni katika hali ambayo hali ya afya ya Sheikh Zakzaki imekuwa ikizorota kila uchao na hasa katika siku za karibuni kwa kadiri kwamba ofisi ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria IMN, imekuwa ikitoa taarifa za mara kwa mara ikitahadharisha kuhusu suala hilo. Hata kama mashinikizo ya Waislamu hatimaye yaliifanya serikali ya Abuja ikubali apelekwe nchini India mwezi Agosti 2019 kwa ajili ya matibabu lakini kutoshirikiana serikali ya New Delhi kwa lengo la kupewa matibabu aliyoyahitaji Sheikh Zalzaki, kulimlazimu arejee nchini Nigeria na kuangukia tena mikononi mwa wanajeshi wasio na huruma wa nchi hiyo.

Katika miezi ya karibuni, kuenea virusi vya corona nchini Nigeria kumehatarisha hata zaidi hali ya afya ya Sheikh Zakzaki pamoja na mkewe. Watawala wa Nigeria si tu kwamba hawamwandalii Sheikh Zakzaki mazingira yanayofaa ya karantini bali hivi karibuni kulisambazwa ripoti kuwa walikuwa na lengo la kumuweka mtu aliyeathirika na virusi vya corona karibu naye ili amuambukize, suala lililopingwa na kulalamikiwa vikali na wafungwa.

Kwa vyovyote vile Waislamu wa Nigeria wamekuwa wakikabiliwa na mashinikazo makubwa kutoka kwa viongozi na maafisa wa jeshi la Nigeria katika miaka ya karibuni, na hasa baada ya kutiwa nguvuni Sheikh Zakzaki. Serikali imepiga marufuku mikusanyiko yote ya Waislamu na wanaoshiriki kwenye mikusanyiko kama hiyo ya kidini hukabiliwa na ukandamiaji mkali wa maafisa usalama. Kwa mtazamo wa viongozi wa Nigeria Sheikh Zakzaki ni kiungo muhimu katika kuleta umoja na mshikamano wa Waislamu wa Nigeria na hii ni katika hali ambayo baadhi ya viongozi hao wanashinikizwa na serikali za kigeni zikiwemo za Marekani na Israel ili waendelee kuwatenganisha Waislamu na kutowashirikisha katika mfumo wa siasa na uchumi wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Waislamu wa India wakiandamana kumtetea Sheikh Zakzaki

Hata kama mashinikizo ya viongozi wa Nigeria yangali yanaendelea kwa ajili ya kumfuta kabisa Sheikh Zakzaki, lakini si Waislamu wa nchi hiyo tu bali fikra za waliowengi katika ulimwengu wa Kiislamu zinapinga vikali siasa hizo za serikali ya Abuja na kutaka mwanazuoni huyo wa Kiislamu aachiliwe mara moja.

Akigusia suala hilo, Maqsud Hussein Domki, Msemaji wa Chama cha Majlisi ya Umoja wa Waislamu wa Pakistan amesema: Zakzaki anapendwa na mamilioni ya Waislamu ulimwenguni, Waislamu ambao hawatasahau kujitolea na mchango wake mkubwa alioutoa katika njia ya kueneza dini tukufu ya Uislamu barani Afrika.

Tags