Nov 26, 2020 11:00 UTC
  • Walibya wakubaliana kuitisha kikao kingine; safari hii ndani ya Libya

Wawakilishi wa makundi mbalimbali ya Libya wanaoshiriki katika kikao cha mjini Tangier, Morocco, wamekubaliana kuitisha kikao kingine katika mji wa Gadamis ndani ya Libya ili kujadiliana suala la kuunganisha mabunge ya nchi hiyo.

Televisheni ya al Jazeera ya Qatar imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, wawakilishi wa makundi ya Libya wanaoshiriki wa kikao cha mashauriano cha mjini Tangier, Morocco, wamekubaliana kimsingi juu ya wajibu wa kuwa na bunge moja lenye idadi inayokubalika ya wabunge na lenye nguvu za kuchukua maamuzi muhimu ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, wabunge 120 wa Libya wamefanya kikao cha faragha katika mji wa Tangier wa kaskazini mwa Morocco na kujadiliana suala la kuyaunganisha mabunge mawili ya Libya na kuwa bunge moja.

Tripoli mji mkuu wa Libya

 

Siku chache zilizopita, mbunge mmoja wa Libya alinukuliwa akisema kuwa, wabunge wa nchi hiyo wanajiandaa kuanza mazungumzo kwa ajili ya kuyaunganisha mabunge mawili ya nchi hiyo yenye makao yao mashariki na magharibi mwa Libya. Mbunge huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema, wabunge wa mabunge hayo yenye makao yao katika miji ya Tobruk na Tripoli  wanajiandaa kushiriki kikao maalumu cha kujadili suala hilo katika mji wa bandari wa Tangier nchini Morocco.

Jumatatu ya tarehe 23 mwezi huu wa Novemba pia, makundi hasimu ya Libya yaliendelea na awamu ya pili ya mazungumzo yao ya kujadiliana njia za kiutaalamu za kuunda serikali ya mpito ambayo itaongoza hadi utakapofanyika uchaguzi mkuu mwezi Disemba 2021.

Mjumbe maalumu wa hivi sasa wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya, Stephanie Williams, ndiye aliyeongoza mazungumzo hayo ya siku ya Jumatatu yaliyofanyika kwa njia ya Intaneti baada ya duru ya kwanza ya mazungumzo hayo huko Tunisia kushindwa kutangaza mamlaka ya kusimamia mchakato wa kuunda serikali hiyo ya mpito. Mazungumzo hayo ya Tunisia yaliwashirikia wajumbe 75 wa makundi mbalimbali hasimu ya Libya.

Tags