Nov 26, 2020 11:42 UTC
  • Waziri Mkuu wa Ethiopia atoa amri ya kushambuliwa makao makuu ya Tigray

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed ametoa amri ya kushambuliwa makao makuu ya jimbo la Tigray, la kasikazini mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa televisheni ya Sky News, amri ya Waziri Mkuu wa Ethiopia ya kushambuliwa Mek'ele, makao makuu ya jimbo la Tigray imetolewa leo Alkhamisi kwa shabaha ya kumaliza uasi wa wanamgambo wa Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray.

Kabla ya hapo, Abiy Ahmed alikuwa amewapa viongozi wa harakati hiyo muda wa masaa 72 wajisalimishe vinginevyo atatoa amri ya kushambuliwa makao makuu ya jimbo hilo.

Muda huo ulimalizika jana Jumatano huku viongozi wa waasi wakiwa hawakuonesha ishara zozote za kujisalimisha bali wametangaza kuwa wamejiandaa kwa vita.

Kabla ya kutoa amri ya kushambuliwa makao makuu ya jimbo hilo leo Alkhamisi, jana Jumatano Waziri Mkuu wa Ethiopia aliitaka jamii ya kimataifa kujiweka mbali na mgogoro unaoendelea huko Tigray.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed

 

Abiy Ahmed alisema hayo baada ya kutolewa wito wa kusitishwa vita vya Tigray ambapo alisisitiza kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kutoingilia kivyovyote vile mgogoro huo kwani ni suala la ndani ya Ethiopia. Alisema, operesheni ya jeshi la nchi hiyo huko Tigray ni ya 'kuokoa sheria'.

Akizungumza mapema jana, Abiy Ahmed alisema, linapokuja suala la msaada, jamii ya kimataifa inapaswa kukaa kando kwanza mpaka serikali ya Ethiopia iwasilishe ombi la kutaka kusaidiwa.

Juzi Jumanne, kuliripotiwa pia habari iliyosema kuwa, idadi kubwa ya wapinganaji wa Harakati ya Wananchi ya Ukombozi wa Tigray wamejisalimisha kwa vikosi vya serikali ya Ethiopia yakiwa yamebakia masaa machache kabla ya kumalizika muhula wa masaa 72 uliokuwa umetolewa na Waziri Mkuu, Abiy Ahmed.

Tags