Nov 27, 2020 02:30 UTC
  • Misri yaionya Israel kwa hatua yake ya kuendeleza ujenzi wake wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

Serikali ya Misri imeuonya utawala haramu wa Israel kwa hatua yake ya kutaka kujenga vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina unazozikalia kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Misri imeeleza kuwa, hatua ya Israel ya kujenga vitongoji vipya katika ardhi za Palestina unazozikaklia kwa mabavu itahatarisha usalama na uthabiti wa eneo la Asia Magharibi.

Kupasisha uamuzi wa kujenga vitongoji vipya huko Quds Mashariki inayokaliwa kwa mabavu na Israel ni tishio kwa amani na usalama wa eneo, imeeleza sehemu moja taarifa hiyo ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Misri.

Kadhalika Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Misri imelaani hatua ya Israel ya kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika maeneo mengine ya ardhi za Palestina na kueleza kwamba, hatua hiyo inakiuka wazi sheria na maazimio ya kimataifa.

Vitongoji haramu vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu

 

Juzi serikali ya Jordan nayo ililaani vikali hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kuafikii ujenzi wa nyumba mpya 540 katika eneo la Quds Mashariki unalolikalia kwa mabavu na kuitaka jamii ya kimataifa iushinikize utawala huo ghasibu ili usitishe ujenzi wake wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina.

Huko nyuma pia Umoja wa Ulaya umewahi kueleza upinzani wake dhidi ya ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni katika ardhi za Palestina na hata kuutaka utawala ghasibu wa Israel usitishe ujenzi huo.

Hata hivyo uungaji mkono wa Marekani kwa Israel umekuwa ukiupa kiburi utawala huo cha kuendelea na siasa zake za kidhalimu dhidi ya Wapalestina.

Tags