Nov 27, 2020 12:29 UTC
  • Ethiopia: Baada ya siku chache, Tigray itakuwa imedhibitiwa kikamilifu

Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia ametangaza kuwa vikosi vya jeshi la nchi hiyo vimeshajiandaa ili kuhakikisha baada ya siku chache tu linaudhibiti kikamilifu mji mkuu wa eneo la Tigray, Mekelle.

Kenea Yadeta ameongeza kuwa, hadi sasa wameshatwaa asilimia 70 hadi 80 ya silaha zilizokuwa mikononi mwa wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi wa Watu wa Tigray na kwamba silaha zingine zimeteketezwa na wapiganaji wengi wa harakati hiyo wameuawa.

Mapigano makali kati ya jeshi la Ethiopia na vikosi vya wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Trgray (TPLF) yalianza tarehe 4 Novemba kwa hujuma ya kijeshi iliyoanzishwa na jeshi la serikali kuu ya Addis Ababa baada ya Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed kuwatuhumu wapiganaji wa TPLF kwamba wameshambulia vikosi vya jeshi la serikali.

Wapiganaji wa TPLF

Serikali ya Ethiopia imekataa upatanishi wa Umoja wa Afrika uliotoa mwito wa kufanyika mazungumzo ya mapema baina ya pande mbili kuhusiana mapigano hayo yanayojiri katika eneo la Tigray.

Baada ya Abiy Ahmed kuingia madarakani mwaka 2018 alianzisha muungano mpya wa kisiasa ambao jamii ya Watigray ilikataa kujiunga nao.

Awali waziri mkuu huyo wa Ethiopia alitoa onyo kwa viongozi wa eneo la Tigray kwamba wasipojisalimisha katika muda wa masaa 72, ambayo yameshamalizika, watakabiliwa na mashambulio makali.

Waziri wa Ulinzi wa Ethiopia Kenea Yadeta amedai pia kwamba wamefanikiwa kuzuia kitisho dhidi ya uwepo wa Ethiopia na pia kutokea mgogoro mkubwa wa hali mbaya ya kibinadamu nchini humo.../

 

Tags