Nov 29, 2020 12:23 UTC
  • Walioambukizwa COVID-19 barani Afrika wapindukia milioni 2.1

Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa cha Afrika (Africa CDC) kimesema, hadi kufikia jana Jumamosi idadi ya maambukizi ya virusi vya COVID-19 au corona barani humo imefikia 2,137,871, na watu 51,248 wamefariki dunia kutokana na virusi hivyo.

Africa-CDC imeongeza kuwa watu 1,807,531 walioambukizwa COVID-19 kote Afrika wamepona.

Taarifa hiyo imezitaja nchi za Afrika zenye kesi nyingi za COVID-19 kuwa ni pamoja na Afrika Kusini, Morocco, Misri na Ethiopia.

Eneo la kusini mwa Afrika limetajwa kuwa lenye kiwango cha juu zaidi cha maambukizi ya COVID-19 na vifo vinavyotokana na ugonjwa huo huku eneo la kaskazini mwa Afrika likiwa la pili.

Wiki iliyopita Africa-CDC ilizindua kampeni inayoitwa Wiki ya Barakoa Afrika kuanzia Novemba 23 hadi Novemba 30, ikilenga kudumisha na kuongeza uvaaji wa barakoa kama hatua ya kujilinda na virusi vya Corona barani humo.

Kampeni ya kukomesha corona nchini Kenya

Mkurugenzi wa Africa CDC John Nkengasong amesema, hatua muhimu ya kudhibiti kuenea kwa virusi vya corona ni kutekeleza mkakati wa afya ya jamii wa kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara na kutimiza umbali wa kijamii.

Nchi za Afrika ziko kwenye tahadhari kubwa ya kutokea wimbi la pili la mlipuko wa virusi vya corona wakati idadi ya kesi za maambukizi ya virusi hivyo barani humo imepindukia milioni mbili.

Tags