Dec 01, 2020 12:48 UTC
  • Kiongozi wa TPLF huko Tigray, Ethiopia aapa kuendeleza mapigano

Kiongozi wa chama cha TPLF cha eneo la Tigray kaskazini mwa Ethiopia amesema askari wake wanaendelea kupambana na jeshi la serikali, siku mbili baada ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed kutangaza ushindi katika eneo hilo.

Kiongozi wa Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray – TPLF- Debretsion Gebremichael amesema ana azma ya kuendeleza mapigano dhidi ya vikosi vya serikali jambo ambalo limepelekea kuwepo wasi wasi wa mapigano kuendelea.

Jana Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alivipongeza vikosi vyake kwa kuzima uasi kaskazani mwa nchi hiyo. Vikosi vya serikali ya shirikisho viliukamata mji mkuu wa Tigray, Mekelle mwishoni mwa wiki na kutangaza ushindi dhidi ya waasi wa TPLF, ambao ni kundi la wapiganaji lililogeuka kuwa chama cha siasa kilichokuwa na nguvu katika serikali kuu kwa karibu miongo mitatu hadi mwaka wa 2018.

Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed

Ijapokuwa TPLF imesema mji wa Mekelle ulishambuliwa kwa mabomu, Abiy amesema wanajeshi wake hawakutumia makombora na hawakumuua raia hata mmoja jimboni Tigray tangu kuanza kwa operesheni ya kijeshi kujibu shambulizi ambalo inadaiwa lilifanywa kwenye kituo cha kijeshi mnamo Novemba 4. Kiongozi wa TPLF Debretsion Gebremichael amekanusha ripoti kuwa amekimbilia Sudan Kusini.

 

Tags