Dec 02, 2020 07:10 UTC

Chama cha Demokrasia kwa ajili ya Mshikamano wa Mataifa cha nchini Morocco kimetoa tamko rasmi na kusema kuwa, mauaji ya kigaidi ya Dk Mohsen Fakhrizadeh, mwanasayansi wa nyuklia na masuala ya kiulinzi wa Iran ni kitendo cha jinai ambacho kimelifanya faili la vitendo vya kigaidi la utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa zito zaidi.

Chama hicho cha nchini Morocco kimesema kuwa, jinai za kuua wasomi wa ulimwengu wa Kiislamu ni moja ya silaha kuu za utawala wa Kizayuni na ubeberu wa Marekani. Kimesema, maadui wamemuua kigaidi msomi huyo mkubwa wa Iran ili kukwamisha maenedeleo ya kielimu na uwezo wa kiulinzi wa taifa la Iran.

Chama hicho kimeitaka jamii ya kimataifa kutekeleza wajibu wake wa kupambana na jinai na ugaidi wa  kiserikali wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Nchi mbalimbali, vyama, taasisi na makundi tofauti duniani yanaendelea kulaani mauaji ya kigaidi aliyofanyiwa mwanasayansi huyo mkubwa wa nyuklia na masuala ya kiulinzi wa Iran, siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Novemba, 2020.

Maziko ya shahid Mohsen Fakhrizadeh mjini Tehran

 

Siku chache zilizopita, shirika la habari la Iran Press liliripoti kuwa, mauaji ya kigaidi ya shahid Mohsen Fakhrizadeh, mwanasayansi mkubwa wa nyuklia na masuala ya ulinzi wa Iran yalifanywa kwa kutumia bunduki maalumu iliyokuwa ikongozwa kutokea mbali na ambayo ilikuwa imefungwa kwenye gari ya pikapu aina ya Nissan.

Kwa mujibu wa taarifa zilizonukuliwa na Iran Press, silaha hiyo ilikuwa imefungwa kifaa maalumu cha mawasiliano ya kuongozea kutoka mbali kilichotengenezwa Israel, ambapo mara baada ya kunasa tawsira ya sura ya shahid Fakhrizadeh ilianza kufyatua risasi kumlenga mwanasayansi huyo wa nyuklia wa Iran.

Tags