Dec 02, 2020 11:09 UTC
  • Bobi Wine asitisha kampeni zake za urais baada ya kushambuliwa na polisi

Mgombea wa urais nchini Uganda kwa tiketi ya chama cha upinbzani cha NUP Robert Kyagulanyi, anayefahamika zaidi kama Bobi Wine, amesitisha kampeni zake, kufuatia kujeruhiwa kwa maafisa wake wa kampeni na kuharibiwa kwa gari lake Jumanne ya jana.

Kiongozi huyo wa upinzani amesema kuwa, risasi zilifyatuliwa kwenye gari lake na kutoboa matairi ya gari lake na kumfanya asiweze kusafiri tena.

Video zilizosambazwa na timu yake ya kampeni kwenye mitandao ya kijamii zinaonesha kitu ambacho hakikutambuliwa kikilipuka umbali wa mita kadhaa kutoka mahali alipokuwa.

Awali katika eneo la Kayunga, mashariki mwa Kampala, mabomu ya gesi ya kutoa machozi yalitumika kuwatawanya wafuasi wake.

Takriban wiki mbili zilizopita, watu 54 waliuawa wakati wafuasi wa mgombea huyo walipokuwa wakiandamana kudai aachiliwe huru baada ya kukamatwa na polisi katika mkutano wa kampeni.

Bobi Wine mwanasiasa kijana ambaye anaonekana kuwa tishio kwa Rais Museveni

 

Baadaye Bobi Wine alishitakiwa kwa kukiuka masharti ya kukabiliana na janga la corona kwa kukusanya umati wa watu na hatimaye akaachiliwa huru kwa dhamana.

Vikosi vya usalama vimeendelea kuzuia mikutano yake ya kisiasa pamoja na ya wanasiasa wengine wa upinzani.

Katika hotuba yake ya kitaifa Jumapili iliyopita, Rais Yoweri Museveni, aliwatetea polisi na jeshi akisema kuwa hakuna mwanasiasa yeyote ambaye hawezi kuguswa.

Kampeni kwa ajili ya uchaguzi wa mwezi Januari mwakani, zimeendelea kupamba moto huku vyama vya upinzani nchini Uganda vikilalamikia kile vinachokitaja kuwa njama za wazi za vikosi vya usalama dhidi ya wapinzani.