Dec 03, 2020 04:50 UTC
  • Tanzania yatuhumiwa kuwafanyia dhulma wakimbizi kutoka Burundi

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limeituhumu Tanzania katika ripoti yake kwamba, imekuwa ikiamiliana vibaya na wakimbizi kutoka Burundi.

Ripoti ya shirika hilo inasema, maafisa wa usalama nchini Tanzania waliwazuia kwa nguvu, kuwatesa na kuwapoteza wakimbizi 18 wa Burundi tangu mwaka 2019 waliokuwa wanaishi katika kambi mbalimbali katika mkoa wa Kigoma.

Shirika la Human Rights Watch linasema kuwa, hatima ya wakimbizi hao haijulikani na kuna hofu kuwa wakimbizi wengine kutoka Burundi huenda walipitia dhulma na mateso hayo.

Tanzania imekuwa ikitoa hifadhi kwa wakimbizi wa Burundi zaidi ya 150,000 waliokimbilia nchini humo tangu mwaka 2015 baada ya mzozo wa kisiasa wakati wa utawala wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo hayati Pierre Nkurunziza.

Serikali ya Tanzania na Burundi, hazijazungumzia kuhusu ripoti hii.

Wakimbizi wa Burundi wakiwa katika moja ya kambi za wakimbizi mkoani Kigoma tanzania

 

Maafisa wa serikali ya Tanzania na Burundi wamekuwa wakihimiza wakimbizi wa Burundi waliokimbilia nchini Tanzania kurudi nyumbani wakisema kwamba, amani imerejea na hakuna sababu za kuendelea kuishi ukimbizini nchini humo.

Duru kutoka nchini Burundi zinasema kuwa, baadhi ya wakimbizi wamerejea nchini humo kwa hiari yao, na wengine bado wanaendelea kurejea kutoka nchi jirani ya Rwanda.

Huku nyuma pia Tanzania imerwahi kulaumiwa baada ya nchi hiyo ya Afrika Mashariki kutangaza uamuzi wa kuwarejesha nyumbani kwa nguvu wakimbizi wa Burundi walioko nchini humo.