Dec 03, 2020 06:38 UTC
  • Makataa yaliyotolewa na Sudan kwa Marekani kwa ajili ya kupasisha sheria ya kuikinga dhidi ya mashtaka ya ugaidi

Licha ya ahadi chungu nzima zilizotolewa na serikali ya Marekani kwa ajili ya kuondolewa Sudan katika orodha ya nchi zinazotuhumiwa kuunga mkono ugaidi na kuishawishi nchi hiyo ianzishe uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel, lakini hakuna hatua yoyote ya maana iliyochukuliwa na serikali ya Washington katika uwanja huo, jambo ambalo limewakawasirisha viongozi wa Khartoum.

Abdul Fattah al-Burhan, Mkuu wa Baraza la Utawala la Sudan ametoa tahadhari kuhusu suala hilo na kusema iwapo sheria ya kuikinga Sudan kutokana na tuhuma za ugaidi haitapasishwa na Congress ya Marekani kufikia mwishoni mwa mwezi huu wa Disemba, basi mwenendo wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel utasimama. Marekani iliiweka Sudan katika orodha ya nchi zinazodaiwa kuunga mkono ugaidi mwaka 1993 katika kipindi cha utawala wa Rais Bill Clinton.

Katika kipindi cha mwisho cha utawala wake, Rais Omar Bashir wa Sudan alifanya juhudi kubwa za kutaka nchi hiyo iondolewe katika orodha hiyo ya Marekani, kwa kujaribu kujikurubisha kwa Marekani na washirika wake katika eneo, ikiwemo kujiunga nchi hiyo na muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya Yemen. Licha ya kujikurubisha na kujipendekeza huko kwa Marekani lakini Sudan haijafanikiwa kuondolewa katika orodha hiyo ya ugaidi.

Kufuatia matukio ya kisiasa ya 2019 nchini Sudan, serikali ya muda ya nchi hiyo ilianza kufuatilia kwa karibu suala la kuondolewa jina la nchi hiyo katika orodha hiyo ya ugaidi ili ipate kunufaika na misaada pamoja na mikopo ya kifedha kutoka mashirika ya kimataifa kwa madhumuni ya kuimarisha uchumi wake. Licha ya mazungumzo mengi yaliyofanyika katika uwanja huo lakini viongozi wa Marekani hawajakubali kuitoa nchi hiyo kwenye orodha hiyo ya nchi zinazotuhumiwa kuunga mkono ugaidi.

Congress ya Marekani

Katika miezi michache iliyopita na kufuatia kubadilika kwa siasa za kigeni za Marekani sambamba na juhudi za Rais Donald Trump za kuzishawishi nchi za Kiarabu zianzishe uhusiano wa kawaida na utawaka wa kibaguzi wa Israel, viongozi wa Washington wamekuwa wakifanya juhudi kubwa za kutumia vibaya udhaifu wa Sudan ili kufikia malengo yao haramu katika eneo. Kwa msingi huo wameishurutisha Sudan ianzishe uhusiano wa kawaida na Israel ili ipate kuondolewa katika orodha hiyo.

Katika miezi miwili iliyopita Washington imefanikiwa kuzishawishi nchi mbili za Kiarabu za Imarati na Bahrain zianzishe uhusiano huo na utawala haramu wa Tel Aviv na kisha Sudan nayo ikashawishiwa ijiunge na nchi hizo katika kuanzisha uhusiano wa kawaida na Israel kwa ahadi ya kuondolewa katika orodha ya nchi zinazounga mkono ugaidi. Viongozi wa Khartoum wanadai kuwa wamelazimika kuanzisha uhusiano na utawala huo wa Kizayuni kutokana na mashinikizo ya Marekani na washirika wake.

Licha ya kutaka kutolewa kwenye orodha inayojadiliwa, viongozi wa Sudan pia wametoa masharti mengine matatu kabla ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Tel Aviv. Masharti hayo ni Sudan kudhaminiwa ngano na nishati ya thamani ya dola bilioni 1.2, kupewa mkopo wa dola bilioni mbili kwa ajili ya kuimarisha uchumi wake na Washington kuisaidia kifedha Sudan kwa muda wa miaka mitatu ijayo.

Licha ya makubaliano yaliyofikiwa na pande mbili katika uwanja huo, lakini Marekani si tu kwamba imekataa kutekeleza ahadi zake bali mechukua hatua ya kurefusha vikwazo dhidi ya nchi hiyo ya Kiafrika.

Mark Knoller mwansidhi wa shirika la CBS la Marekani ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba: Licha ya kuwepo mapatano ya Sudan na Israel kwa ajili ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na pia kufutwa jina la Sudan katika orodha ya Marekani ya nchi zinazounga mkono ugaidi, lakini Trump ameijulisha Congress kuwa jina la Sudan litaendelea kuwa kwenye orodha hiyo kwa muda wa mwaka mmoja mwingine kutokana na hali ya dharura ya kitaifa kuhusu Sudan.

Benjamin Netanyahu wa Israel (kushoto) na Abdul Fattah al-Burhan wa Sudan

Kufikia sasa hakuna hatua yoyote iliyochukuliwa na Washington kwa ajili ya kufuta jina la Sudan katika orodha ya nchi zinazotuhumiwa kuunga mkono ugaidi. Ni kutokana na hali hiyo ndipo viongozi wa Khartoum wakaonya kwamba iwapo kufikia mwishoni mwa mwezi huu, Congress ya Marekani haitakuwa imepitisha sheria ya kuikinga Sudan kutokana na mashtaka ya wahanga wa vitendo vya ugaidi, basi nayo itasimamisha mwenendo wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa kibaguzi wa Israel.

Viongozi wa Marekani ambao, hasa katika kipindi hiki cha utawala wa Trump, wamekuwa wakitekeleza siasa za upande mmoja na kimaslahi kupitia nara ya 'Marekani Kwanza' na hivyo kujitoa katika mikataba muhimu ya kimataifa, pia wamekuwa wakitumia vibaya hali mbaya na dhaifu ya kisiasa na kiuchumi ya Sudan kwa ajili ya kufikia malengo yao katika eneo.

Pamoja na hayo inaonekana kuwa viongozi wa Sudan wana muda mfupi sana wa kuchukua uamuzi iwapo watatia saini mkataba rasmi wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel au la.

Tags