Dec 03, 2020 07:29 UTC
  • Mjumbe wa UN: Libya ina

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya ametahadharisha kuwa, kuwepo wapiganaji na mamluki wasiopungua 20,000 wa kigeni nchini humo kunaifanya "hali iwe mbaya sana" huku silaha zikiendelea kumiminika pia katika nchi hiyo ya Afrika Kaskazini iliyoharibiwa vibaya na vita.

Stephanie Williams amelieleza jopo la wajumbe 75 wa kikao cha Jukwaa la Mazungumzo ya Kisiasa ya Libya kilichofanyika kwa njia intaneti kwamba "huo ni ukiukaji wa kutisha wa mamlaka ya kujitawala ya Libya... na pia ni ukiukaji wa wazi kabisa wa vikwazo vya silaha."

Kauli hiyo ya Bi Williams imekuja kutokana na kutopiga hatua mpango wa kuwaondoa wapiganaji wa kigeni pamoja na mamluki walioko Libya, ambao ni sehemu ya makubaliano ya ustishaji vita yaliyosainiwa mwezi Oktoba.

Makubaliano hayo ya usitishaji mapigano yalitoa muhula wa miezi mitatu kwa maelfu ya mamluki na wapiganaji wa kigeni wakiwemo raia wa Russia, Syria, Sudan na Chad kuondoka katika ardhi ya Libya, ambao kwa mujibu wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa walipelekwa huko na pande hasimu zinazopigana nchini humo.

Mjumbe huyo wa UN vilevile ametoa indhari kwamba, watu milioni moja na laki tatu kati ya Walibya wote milioni sita na laki nane watakuwa wanahitaji misaada ya kibinadamu ifikapo mwezi ujao wa Januari. 

Viongozi wa pande hasimu Libya: Fayez al Sarraj (kulia) na Khalifa Haftar

Jopo hilo la wajumbe 75 linajaribu kuzishawishi pande zinazopigana vita nchini Libya zikubaliane kuhusu utaratibu utakaotumiwa kuunda serikali ya mpito itakayoiongoza nchi hiyo kuelekea uchaguzi wa rais na bunge uliopangwa kufanyika Desemba 2021.

Kikao hicho ni sehemu ya jitihada za Umoja wa Mataifa za kumaliza vita na machafuko katika nchi hiyo inayozalisha mafuta kwa wingi, ambayo ilitumbukia kwenye lindi la vita na mapigano tangu alipouawa kiongozi wake wa zamani Muammar Gaddafi mwaka 2011 katika vuguvugu la wananchi lililopewa msukumo na uvamizi wa shirika la kijeshi la NATO likishirikiana na madola ya Magharibi.

Tangu mwaka 2015, Libya imekuwa chini ya udhibiti wa makundi yanayobeba silaha, ikiwa imegawanyika katika maeneo makuu mawili yanayoendeshwa na pande mbili hasimu, moja ikiwa ni Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa (GNA) inayotambuliwa rasmi na Umoja wa Mataifa ambayo makao yake yako katika mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli, na nyingine ni ile iliyoko katika mji wa mashariki wa Tobruk ambayo inaungwa mkono na kundi linalojiita Jeshi la Taifa la Libya (LNA) linaloongozwa na jenerali mwasi Khalifa Haftar.../

 

Tags