Dec 03, 2020 07:52 UTC
  • Ofisi ya Sheikh Zakzaky: Boko Haram haliwakilishi Waislamu kwa namna yoyote ile

Ofisi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imelaani mauaji ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo yaliyofanywa na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Boko Haram.

Taarifa iliyotolewa na ofisi ya kiongozi huyo wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria, mbali na kulaani mauaji ya makumi ya wakulima wasio na hatia waliouliwa na kundi hilo la kigaidi katika jimbo la Borno kaskazini mashariki mwa nchi, imesisitiza pia kuwa utawala wa Muhammadu Buhari ndio msababishaji wa hali inayotawala hivi sasa ndani ya Nigeria.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya ofisi ya Sheikh Zakzaky, kundi la kigaidi la Boko Haram limeundwa na vikosi vyenye nia ya kuharibu na kufuta sura halisi ya Uislamu ya kupenda amani na kwamba kuongezeka mashambulio ya kigaidi na utekaji nyara ni mfano wa karibuni kabisa wa hatua zinazochukuliwa na utawala wa Buhari.

Ofisi ya Sheikh Ibrahim Zakzaky imeeleza katika taarifa hiyo kwamba, badala ya utawala wa Nigeria kulinda roho na mali za watu ambalo ni jukumu la kila serikali unafanya kila njia kuua na kuangamiza maisha ya watu wasio na kosa lolote.

Sheikh Ibrahim Zakzaky

Siku ya Jumapili iliyopita, magaidi wa kundi la ukufurishaji la Boko Haram walishambulia kijiji cha Garin Kwashebe katika jimbo la Borno na kufanya mauaji ya kikatili ya halaiki ya wakulima wasiopungua 110.

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imezungumzia pia ukandamizaji wa wafuasi wa Sheikh Ibrahim Zakzaky unaofanywa na vikosi vya usalama na kueleza kwamba, wafuasi hao wanaoandamana kwa amani kulalamikia kuendelea kuwekwa kizuizini kinyume cha sheria kiongozi wao huyo wa kidini wanashambuliwa kikatili na vikosi hivyo.

Katika miezi ya karibuni, wananchi wa Nigeria wamefanya maandamano kadhaa ya amani katika miji mbalimbali ya nchi hiyo kutaka Sheikh Zakzaky aachiliwe huru lakini kila mara vikosi vya usalama vimetumia mkono wa chuma kuzima maandamano hayo.

Sheikh Ibrahim Zakzaky na mkewe walikamatwa na kuwekwa kizuizini Desemba 13, 2015 katika uvamizi na shambulio la kinyama lililofanywa na askari wa jeshi la Nigeria katika Husainiyya ya mji wa Zaria.

Katika hujuma hiyo, askari wa jeshi la Nigeria waliwafyatulia risasi na kuwaua shahidi mamia ya Waislamu waliokuwa wamekusanyika kwenye Husainiyya hiyo wakiwemo watoto watatu wa kiume wa Sheikh Zakzaky.../