Dec 03, 2020 11:06 UTC
  • Algeria yautaka Umoja wa Afrika kutekeleze majukumu yake kuhusu Sahara Magharibi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria amesema kuwa Algiers inasikitishwa mno na hali ya Sahara Magharibi hususan matukio yaliyoshuhudiwa hivi karibuni na ameutaka Umoja wa Afrika AU utekeleze ipasavyo majukumu yake katika eneo hilo.

Shirika la habari la FARS limemnukuu Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Sabri Boukadoum, akisema hayo katika kikao cha Baraza la Utendaji la Umoja wa Afrika AU na kuongeza kuwa, uzorotaji wa kupindukia wa mchakato wa kisiasa unaosimamiwa na Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kutatua mgogoro wa Sahara Magharibi ndio uliopelekea kuongezeka mateso kwa wananchi wa eneo hilo hasa kwa kuzingatia kuwa hakuna upeo wowote unaoshuhudiwa katika mazungumzo ya kisiasa ya kuainisha mustakbali wa Sahara Magharibi.

Amesema, kuwavamia na kuwashambulia raia na watu wa kawaida wa eneo la al Guerguerat huko Sahara Magharibi ni changamoto kubwa inayodhoofisha juhudi za kuleta amani na usalama katika eneo hilo na ameutaka Umoja wa Afrika uchukue msimamo wa wazi na imara wa kuzuia kuendelea matukio hayo hatari.

Sahara Magharibi

 

Kwa mujibu wa makubaliano ya kusimamisha vita ya mwaka 1991, eneo la al Guerguerat linapaswa kuwa ukanda wa amani usio na silaha na kwamba ukuta uliojengwa na Morocco katikati ya muongo wa 80 ndio mpaka wa ukanda huo. Hivi sasa ukanda huo unasimamiwa na kikosi maalumu cha Umoja wa Mataifa.

Tarehe 13 Novemba mwaka huu, harakati ya Polisario ya kupigania ukombozi wa Sahara Magharibi ilitangaza kusimamisha makubaliano ya eneo hilo baada ya jeshi la Morocco kufungua kwa nguvu njia ya kuingilia nchi jirani ya Mauritania iliyokuwa imefungwa na harakati hiyo.

Tags