Dec 03, 2020 11:06 UTC
  • Rais wa Ghana atangaza mapumziko rasmi siku ya uchaguzi mkuu nchini humo

Rais wa Ghana, ameitangaza tarehe 7 mwezi huu wa Disemba kuwa ni siku ya mapumziko nchini humo ili kurahisisha zoezi la uchaguzi mkuu na kuruhusu ufanyike katika mazingira bora kabisa.

Katika taarifa yake, Rais Nana Addo Dankwa Akufo-Addo amesema, Disemba 7, 2020 itakuwa siku ya mapumziko ili kuhakikisha uchaguzi mkuu unafanyika kwa njia salama na bora wakati huu wa maambukizo ya COVID-19. Siku hiyo itakuwa ya mapumziko ili kuruhusu wapiga kura wachunge protokali zote za kiafya na kushiriki katika zoezi hilo katika mazingira salama na yasiyo hatarishi kwa afya zao.

Vile vile rais huyo Ghana amefuta sherehe za kila mwaka za Siku ya Mkulima mwaka huu ambayo ilikuwa iadhimishwe kesho Ijumaa. Sababu ya kufutwa sherehe hizo za kesho kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni kwamba Jumatatu tayari imeshatangazwa kuwa ni siku ya mapumziko kwa ajili ya uchaguzi.

Zaidi ya watu milioni 17 wamejiandikisha katika daftari la wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa rais na Bunge la nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika lenye wabunge 275. 

John Dramani Mahama

 

Mchuano mkubwa katika uchaguzi huo upo baina ya wagombea wawili wakuu, rais wa hivi sasa Akufo-Addo na rais wa zamani wa nchi hiyio, John Dramani Mahama.

Yeyote atakayeshinda kati ya wagombea hao wawili, atahudumu kwa kipindi kimoja tu cha urais kwani kwa mujibu wa Katiba ya Ghana, mtu hawezi kuwa rais kwa zaidi ya vipindi viwili. Uchaguzi wa Disemba 7, 2020 utakuwa ni wa nane mkuu kufanyika nchini humo tangu ulipoanza mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 katika nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.