Dec 15, 2020 13:24 UTC
  • Hofu yatanda baada ya Somalia kutuma wanajeshi katika mpaka na Kenya

Masaa machache baada ya Somalia kutangaza kukata uhusiano wa kidiplomasia na Kenya, Jeshi la Kitaifa la Somalia (SNA) limetuma idadi kubwa ya askari katika eneo moja la mpaka wa pamoja wa nchi hizo mbili.

Kwa mujibu wa taarifa, wakaazi wa Kaunti ya Mandera wameripoti kuona idadi kubwa ya askari wa SNA wakiwa wanajiweka katika maeneo ya kistratijia ya mpaka wa nchi mbili.

Baadhi ya wakaazi wa eneo hilo wamelazimika kukimbia nyumba zao baada ya kuingiwa na hofu walipoona magari ya deraya  ya Jeshi la Kitaifa la Somalia mapema leo asubuhi.

Mapema Jumanne, Waziri wa Habari wa Somalia Osman Dubbe alitangaza katika televisheni ya kitaifa kuwa nchi yake imekata uhusiano wa kidiplomasia na Kenya.

Dubbe amedai kuwa Kenya imekuwa ikiingilia mambo ya ndani ya Somalia mara kwa mara na kwamba Nairobi inakiuka mamlaka ya kijitawala Somalia.

Uamuzi huo wa Somalia umekuja wakati Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alikiwa mwenyeji wa Rais wa Somaliland, Muse Bihi mjini Nairobi. Eneo la Somaliland lilijitangazia uhuru kamili kutoka Somalia  mwaka 1991 lakini serikali ya Somalia haitambui kujitenga eneo hilo.

Wafanyabiashara katika mji wa Mandera wanasema wataathiriwa vibaya na msuguano wa Kenya na Somalia kwani wao hutegemea bidhaa kutoka Mogadishu kutokana na kuwa eneo hilo liko mbali sana na Nairobi.

Wakati hayo yakijiri serikali ya Kenya imesema imeunda kamati maalumu kuchunguza chanzo cha msuguano baina yake na Somalia.

Msemaji wa serikali ya Kenya kanali mstaafu Cyrus Ogina amesema kamati hiyo itatafuta njia za kidiplomasia kutatua tatizo lililojitokeza.

 

Tags