Dec 20, 2020 03:24 UTC
  • Marekani yaondoa askari wake Somalia na kuwapeleka katika nchi nyingine za Afrika

Jeshi la Marekani limezindua operesheni ya kuwaondoa askari wake kutoka Somalia na kuwapeleka katika nchi nyingine za Afrika.

Kamandi ya Jeshi la Marekani Barani Afrika (AFRICOM) imetangaza kuwa, manowari ya nchi hiyo kwa jina la USS Africa Hershel Woody Williams mapema jana Jumamosi ilianza kuwasafirisha wanajeshi hao wa US na kuwapeleka katika nchi nyingine za Afrika.

Askari hao wa Marekani wamekuwepo nchini Somalia kwa kisingizio cha kuvisaidia vikosi vya serikali ya Mogadishu katika operesheni zake za kukabiliana na wanamgambo wa kundi la kigaidi la al-Shabaab.

Hivi karibuni, maafisa wa kijeshi wa US walitangaza kuwa, asilimia kubwa ya askari wake walioko Somalia watakuwa wameondoka nchini humo ifikapo tarehe 15 Januari ya mwaka ujao wa 2021.

Askari vamizi wa Marekani barani Afrika

Awali Rais Donald Trump aliitaka Wizara ya Ulinzi ya nchi hiyo (Pentagon) sambamba na kuondoa nchini Somalia sehemu kubwa ya askari hao na kuwarejesha nyumbani, iunde kikosi kidogo kitakachobakia katika mji mkuu Mogadishu.

Ripoti zinaonyesha kuwa, kwa sasa Marekani ina askari 700 nchini Somalia. Viongozi wa mataifa ya Afrika ikiwemo Somalia daima wamekuwa wakitaka majeshi vamizi ya Marekani yaondoke katika nchi zao.

Tags