Dec 20, 2020 15:30 UTC
  • Mivutano yazidi kupamba moto huku Somalia ikiituhumu Kenya kuwapatia silaha wanamgambo

Serikali kuu ya Somalia imeionya Kenya juu ya matokeo mabaya ya hatua yake ya kuweka wanajeshi wake katika mji wake wa mpakani wa Mandera na kulipatia silaha kundi moja la waasi kwa lengo la kuvuruga uthabiti ndani ya Somalia.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Habari ya Somalia imesema, serikali hiyo inazo taarifa kuhusu hatua ya jeshi la Kenya ya kusambaza wanamgambo ndani ya mji huo na kuwapatia silaha ili washambulie kambi za jeshi la Somalia katika mji wa Beled Hawo.

Serikali kuu ya Mogadishu vilevile imeitahadharisha Kenya na matokeo mabaya ya hatua yoyote itakayochukua kudhoofisha uthabiti katika eneo la Pembe ya Afrika na kuitaka iangalie upya sera zake za kuingilia masuala ya ndani ya Somalia ambazo zitapelekea kuvurugika uthabiti na amani ya eneo hilo.

Siku ya Jumanne iliyopita, serikali ya Somalia ilitangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Kenya likiwa ni jibu kwa kile ilichokieleza kuwa ni ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya kisiasa unaofanywa na nchi hiyo na uingiliaji wake wa wazi katika masuala ya utawala ya Somalia.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya (kulia) na Rais  Mohamed Abdullahi Mohamed 'Farmaajo' wa Somalia

Serikali kuu ya Mogadishu ilitangaza kuwafukuza wanadiplomasia wote wa Kenya na kuagiza wanadiplomasia wake wote walioko Nairobi warudi nyumbani ndani ya siku saba kuanzia siku hiyo ya tarehe 15 Desemba.

Kabla ya hapo serikali kuu ya Mogadishu iliituhumu Kenya kuwa imekuwa ikimshinikiza sana rais wa Jubaland Ahmed Mohamed Islaam Madobe atekeleze mambo yenye maslahi kisiasa na kiuchumi kwa nchi hiyo na hivyo kudhoofisha makubaliano ya kisiasa yaliyosainiwa hivi karibuni nchini Somalia, ukiwa ni ukiukaji wa taratibu za kidiplomasia.

Kwa mujibu wa Serikali kuu ya Somalia, kutokana na uingiliaji wa kisiasa wa Kenya katika masuala ya ndani ya nchi hiyo, rais wa eneo la Jubaland amehalifu makubaliano yaliyosainiwa Septemba 17 mjini Mogadishu kuhusu uchaguzi wa eneo hilo.../

Tags