Dec 21, 2020 08:23 UTC
  • AU yataka Kenya na Somalia zitumie mazungumzo kusuluhisha mzozo baina yao

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ametoa mwito kwa Kenya na Somalia kufuata njia ya mazungumzo kuutafutia ufumbuzi mgogoro uliopo baina ya pande mbili.

Moussa Faki Mahamat amesema mvutano wa kidiplomasia baina ya nchi mbili hizo jirani unaitia wasi wasi mkubwa AU. Amesema nchi mbili hizo zina historia ndefu ya ujirani mwema, na kukumbusha kuwa Kenya mbali na kuwa mwenyeji wa idadi kubwa ya wakimbizi wa Kisomali, lakini pia imetuma wanajeshi wake kuungana na Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja huo nchini Somalia AMISOM katika kupambana na wanamgambo wa al-Shabaab.

Mzozo huo wa kidiplomasia baina ya Kenya na Somalia ulikuwa moja ya ajenda kuu katika Kikao cha Dharura cha Jumuiya ya Kikanda IGAD kilichofanyika jana nchini Djibouti.

Mkutano huo uliotishwa na Abdalla Hamdok, Waziri Mkuu wa Sudan ambaye ndiye mwenyekiti wa sasa wa IGAD, ulihudhuriwa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, wenzake wa Djibouti Ismail Omar Guelleh na Mohamed Abdullahi wa Somalia, pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed.

Jumanne iliyopita, serikali ya Somalia ilitangaza kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Kenya likiwa ni jibu kwa kile ilichokieleza kuwa ni ukiukaji wa mara kwa mara wa makubaliano ya kisiasa unaofanywa na nchi hiyo na uingiliaji wake wa wazi katika masuala ya utawala ya Somalia.

Mogadishu ilitangaza kuwafukuza wanadiplomasia wote wa Kenya na kuagiza wanadiplomasia wake wote walioko Nairobi warudi nyumbani ndani ya siku saba kuanzia siku hiyo ya tarehe 15 Desemba.

Tags