Dec 23, 2020 00:54 UTC
  • Somalia yaafiki kurejesha uhusiano na Kenya baada ya mashinikizo ya IGAD

Somalia imeafiki kurejesha uhusiano wake na Kenya kufuatia mashinikizo ya Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Mashariki mwa Afrika na pembe ya Afrika IGAD.

Duru zimearifu kuwa katika kikao cha IGAD kilichofanyika huko Djibouti mapema wiki hii, viongozi waliohudhuria kikao hicho waliishinikiza Somalia isitishe hatua zitakazoshadidisha taharuki na uhasama katika eneo.

Waziri wa mambo ya nje wa Somalia Mohamed Abdirizak Mohamud amethibitisha taarifa hizo na kusema nchi yake ilishinikizwa katika kikao hicho cha IGAD kusitisha uhasama na nchi jirani ya Kenya. Mohamud amesema Somalia imekubali ombi lililotolewa na jumuiya hiyo la kutatua mzozo kupitia mazungumzo kwa sharti kwamba iundwe timu ya kutafuta ukweli ya IGAD ili kuchunguza malalamiko ya Somalia. 

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta na mwenzake wa Somalia Mohamed Farmajo wote wawili walikutana pembizoni mwa kikao hicho cha kilele cha 38 cha IGAD, ambapo rais Mohamed ameeleza imani yake kwamba mzozo huo utatatuliwa kwa amani na nchi mbili zitarejesha uhusiano wao wa kibalozi.

Marais wa Kenya, Djibouti na Somalia pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia katika kikao cha IGAD nchini Djibouti

Wiki iliyopita, Somalia ilitangaza kukata rasmi uhusiano wa kidiplomasia na Kenya na kuilaumu Kenya kwa kujaribu kuingilia mamlaka ya kujitawala ya nchi hiyo.

Mzozo baina ya Kenya na Somalia umeanza kuathiri vibaya vita dhidi ya kundi la kigaidi la Al Shabab kwa kuzingatia kuwa Kenya ina askari 3,500 wanaoisaidia Somalia kukabiliana na ugaidi.

Walioshiriki katika kikao hicho cha Djibouti ni pamoja na mwenyeji, Rais Ismail Omar Guelleh,Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya, Rais Mohamed Abdullahi Mohamed wa Somalia, na Rebecca Nyandeng De Mabior, Makamu wa Rais wa Sudan Kusini. Aidha kikao hicho kilihudhuriwa na Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

Tags