Dec 23, 2020 12:23 UTC
  • Al-Shabaab yakiri kumuua chifu wa Wajir Kenya kwa kumkata kichwa

Kundi la kigaidi la al-Shabaab lenye makao yake nchini Somalia limekiri kuwa ndilo lililomteka nyara na kumuua kwa kumkata kichwa chifu mmoja wa kaunti ya Wajir, huko kaskazini mashariki mwa Kenya.

Genge hilo la ukufurishaji limekiri kutekeleza ukatili huo kupitia shirika lake la habari za kipropaganda la Shahada. Kadhalika duru za kiusalama na vyombo vya habari vya Kenya vimetangaza habari hiyo ya kutekwa na kuuawa kwa kuchinjwa Omar Adan Buul, chifu wa lokesheni ndogo ya Gumarey kaunti ya Wajir, katika mpaka wa Kenya na Somalia.

Afisa wa polisi wa Kenya ambaye hakutaka kutaja jina lake ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, "ni kweli chifu huyo aliyetoweka Ijumaa iliyopita amepatikana ameuawa. Kichwa chake kilitupwa barabarani, lakini sehemu nyingine ya kiwiliwili chake haijapatikana."

Afisa mwingine usalama wa Kenya amesema tayari wamekichukua kichwa cha cifu huyo na kukipeleka katika chumba cha kuhifadhi maiti, huku shughuli ya kuusaka mwili wake ikiendelea.

Shambulio la bomu la al-Shabaab huko Wajir Kenya miaka kadhaa nyuma

Magaidi hao wa al-Shabaab walimteka nyara chifu huyo baada ya kushambulia kituo cha polisi katika kaunti ya Wajir Ijumaa iliyopita, mbali na kuwahutubia kwa lazima wakaazi wa kijiji hicho. 

Haya yanajiri wakati huu ambapo mzozo baina ya Kenya na Somalia umeanza kuathiri vibaya vita dhidi ya kundi la kigaidi la al-Shabaab kwa kuzingatia kuwa Kenya ina askari 3,500 wanaoisaidia Somalia kukabiliana na ugaidi.

Tags