Dec 25, 2020 13:11 UTC
  • Marekani kufungua ubalozi mdogo Sahara Magharibi, Morocco

Katika kile kinachoonekana ni muendelezo wa ukiukaji wa sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa, Marekani imetangaza kuwa imeanzisha mchakato wa kufungua ubalozi mdogo katika eneo la Sahara Magharibi, huko kusini mwa Morocco.

Katika ujumbe wake wa Twitter, Mike Pompeo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani amesema kuwa: Tuna furaha kutangaza kuanza mchakato wa kufungua ubalozi mdogo wa Marekani katika eneo la Sahara Magharibi, na pia kuzinduliwa shughuli za ofisi hiyo kwa njia ya intaneti.

Pompeo amedai kuwa, Washington inatazamia kuboresha hali ya kijamii na kiuchumi ya Sahara Magharibi, sambamba na kuwa na maingiliano mazuri na watu wa eneo hilo.

Amesema ofisi hiyo ya intaneti kwa sasa itasimamiwa na ubalozi wa Marekani ulioko mjini Rabat kabla ya kufunguliwa rasmi ubalozi mdogo wa Washington katika eneo hilo. 

Ramani inayoonesha eneo la Sahara Magharibi

Haya yanajiri wiki mbili baada ya Rais wa Marekani anayeondoka, Donald Trump kutangaza kuwa Washington inatambua rasmi kwamba eneo la Sahara Magharibi ni milki ya Morocco, ikiwa ni kujaribu kuhalalisha uamuzi wa nchi hiyo wa kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Uamuzi huo umelaaniwa vikali kimataifa. António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameikosoa Marekani kwa hatua yake hiyo na kusisitiza kuwa, umiliki wa eneo la Sahara Magharibi si kitu cha kutambuliwa rasmi na nchi fulani, kwani maazimio ya UN ndiyo yenye kauli ya mwisho kuhusu eneo hilo.

Tags