Dec 28, 2020 00:21 UTC
  • Jeshi la Kenya lashambulia maficho ya al-Shabaab na kuua kadhaa

Kikosi Maalumu cha Jeshi la Ulinzi la Kenya (KDF) jana Jumapili kilishambulia maficho ya kundi la kigaidi na kitakfiri la al-Shabaab katika Msitu wa Boni kaunti ya Lamu, pwani ya Kenya na kuangamiza wanachama kadhaa wa genge hilo.

Picha ya video za opereseheni hiyo zimesambaa katika mitandao ya kijamii. Haijabainika ni magaidi wangapi wa al-Shabaab wameuawa katika shambulio hilo la jana lakini duru za habari zinasema kwa akali wanachama wanne wa genge hilo wameangamizwa.

Wanajeshi hao wa KDF wamefanikiwa kunasa silaha zilizokuwa mikononi mwa magaidi hao, yakiwemo maguruneti, risasi, radio za mawasiliano na kanda za video.

Inaarifiwa kuwa, genge hilo la kigaidi lilikuwa linakula njama za kutekeleza wimbi la mashambulizi katika pwani ya Kenya katika kipindi hiki cha shamrashamra za sherehe za kufunga mwaka 2020 Miladia.

Wanachama wa al-Shabaab katika Msitu wa Boni, kaunti ya Lamu nchini Kenya

Haya yanajiri chini ya wiki moja baada ya kundi hilo la kigaidi kukiri kuwa ndilo lililomteka nyara na kumuua kwa kumkata kichwa Naibu Chifu mmoja wa kaunti ya Wajir, huko kaskazini mashariki mwa Kenya.

Magaidi hao wa al-Shabaab walimteka nyara afisa huyo wa serikali baada ya kushambulia kituo cha polisi katika kaunti hiyo, ambapo mbali na kuwahutubia kwa lazima wakaazi wa kijiji hicho, waliiba chakula cha msaada cha wakazi wa eneo hilo.

 

Tags