Dec 30, 2020 08:11 UTC
  • Wamorocco wafungua shauri mahakamani la kufutwa mapatano ya kuanzisha uhusiano na Israel

Mratibu wa Kongresi ya Kitaifa ya Kiislamu ya Morocco amesema wamefungua shauri mahakamani la kuangaliwa upya uamuzi uliochukuliwa na serikali ya Rabat wa kufikia mapatano na Israel ya kuanzisha uhusiano wa kawaida wa kisiasa, kidiplomasia, kiuchumi na katika sekta ya utalii.

Khalid al Sufian Wakili na Mratibu wa Kongresi ya Kitaifa ya Kiislamu ya Morocco amewasilisha katika Mahakama ya Rufaa ya nchi hiyo ombi la kuangaliwa upya uamuzi wa serikali ya Rabat wa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni katika nyanja za  kisiasa, kidiplomasia, kiuchumi na utalii. 

Ombi hilo limetilia mkazo ulazima wa kufutwa maagizo yote yaliyotekelezwa na mamlaka ya Morocco na utawala wa Israel na imeelezwa kuwa, maamuzi hayo yanakinzana na katiba ya Morocco, Hati ya Umoja wa Mataifa, Mkataba wa The Hague, na sheria za kimataifa za haki za binadamu.  

Ahmad Wihiman Mkuu wa Taasisi inayopinga kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni  amesisitiza kuwa takwa kuu la makundi ya Morocco ni kufutwa mapatano hayo na si jingine. Amesema suala hilo pia linaungwa mkono na wananchi wa Morocco ambao wanatambua kuwa kadhia ya Palestina ni suala la kitaifa. 

Tags