Jan 02, 2021 07:26 UTC
  • Morocco yasimamisha uhusiano wake na Wazayuni

Duru kadhaa za kidiplomasia zimetangaza kuwa serikali ya Morocco imesimamisha kutangaza kiukamilifu uhusiano wake na utawala wa Kizayuni hadi itakapojua msimamo wa rais ajaye wa Marekani kuhusu Sahara Magharibi.

Gazeti la al Sharq al Awsat limezinukuu duru hizo zikisema kwamba Morocco imesimamisha mchakato wa kuanzisha uhusiano kamili wa kidiplomasia na Israel hadi atakapoingia madarakani Joe Biden huko Marekani na kujua msimamo wake kuhusu Sahara Magharibi.

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, kwa hivi sasa Morocco itatosheka tu na kufungua ofisi ya uhusiano baina yake na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Sahara Magahribi

 

Kabla ya hapo, rais wa hivi sasa wa Marekani, Donald Trump alidai kuwa eneo la Sahara Magharibi ni mali ya Morocco, na suala hilo likatumiwa na viongozi wa Rabbat kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel. Trump alidai kuwa Morocco iliitambua nchi ya Marekani mwaka 1777 hivyo ni bora na sisi tukatambua kuwa, Sahara Magharibi ni eneo la Morocco. Eneo la Sahara Magharibi liko kusini mwa Morocco na limedhibitiwa na nchi hiyo tangu mwaka 1974 baada ya kumailizika ukoloni wa Uhispania katika eneo hilo.

Harakati ya Polisario inayopigania ukombozi wa Sahara Magharibi inaungwa kono na Algeria na baadhi ya nchi za eneo hilo. Gazeti la al Sharaq al Awsat pia limenukuu duru nyingine ya Tel  Aviv na kusema kuwa, timu ya Joe Biden haina haraka kuhusu kutangaza msimamo wake juu ya Sahara Magharibi, jambo ambalo linaitesa sana Morocco.

Morocco ilikuwa nchi ya nne ya Kiarabu kutangaza uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni wa Israel, mwaka ulioisha wa 2020. Nchi nyingine ni Imarati, Bahrain na Sudan.

Tags