Jan 08, 2021 02:43 UTC
  • Mripuko waua watu 7 katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu

Watu wasiopungua 7 wameuawa katika mripuko wa bomu uliotokea katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Shirika la habari la Anadolu limeripoti habari hiyo na kuzinukuu duru za kiusalama za Somalia zikitangaza jana Alkhamisi kwamba, mripuko huo umetokea baada ya basi moja lililokuwa na wanajeshi kukanyaga bomu barabarani na kusababisha vifo vya watu 7.

Duru za kiusalama za Somalia zimethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, waliouawa ni wanajeshi wawili na raia watano waliokuwepo karibu na eneo hilo.

Juzi Jumatano pia gari la Sadiq Adam, msemaji wa jeshi la polisi mjini Mogadishu liliripuliwa kwa bomu na kuua mtu mmoja.

Magaidi wa al Shabab

 

Hadi tunapokea habari hii hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na miripuko hiyo. Hata hivyo mashambulizi kama hayo mara nyingi hufanywa na genge la kigaidi na la ukufurishaji la al Shabab ambalo lilianzisha mashambulizi ya kila upande nchini Somalia mwaka 2004.

Baadaye genge hilo la kigaidi lilijitangaza kuwa ni sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al Qaida na hadi hivi sasa limeshafanya mashambulizi mengi ya kigaidi ndani na nje ya Somalia. Mamia ya watu wameshapoteza maisha yao kutokana na vitendo vya kigaidi vya genge hilo.

Mwaka 2011 serikali ya Somalia ilifanikiwa kulifurusha genge la al Shabab mjini Mogadishu, hata hivyo bado genge hilo lina wafuasi wake katika maeneo mbalimbali ya vijijini huko Somalia na linadhibiti baadhi ya maeneo hayo. 

Tags