Jan 09, 2021 11:22 UTC
  • Uchaguzi wa kwanza nchini Libya mwaka huu wa 2021

Sambamba na juhudi za kidiplomasia zinazofanyika kwa shabaha ya kupata ufumbuzi wa mgogoro wa Libya na hatimaye kufikia mapatano ya kudumu ya kisiasa, kumefanyika uchaguzi wa kwanza wa mabaraza ya miji katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Libya umepongeza zoezi hilo la uchaguzi wa kwanza wa mabaraza ya miji nchini Libya katika mwaka huu wa 2021 na kusifu irada na azma ya kitaifa ya nchi hiyo katika kutumia haki zake za kidemokrasia.

Mazungumzo ya kutafuta amani ya kudumu nchini Libya na kuitisha uchaguzi wa rais kwa shabaha ya kuhamisha madaraka kwa njia za kidemokrasia yanaendelea huku nchi hiyo ikiendelea kusumbuliwa na uingiliaji wa madola ya kigeni katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. Misri na Uturuki zinatambuliwa kuwa wachezaji wakuu katika medani ya siasa za ndani za Libya na katika wiki za hivi karibuni zimezidisha harakati zao nchini humo. 

Wiki kadhaa zilizopita Bunge la Uturuki lilirefusha muda wa majukumu ya jeshi la nchi hiyo huko Libya kwa kipindi kingine cha miezi 18. Sambamba na hayo Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa ya Libya inayoungwa mkono na Uturuki imeimarisha zaidi jeshi lake katika medani ya vita ya Sirte-Al Jufrah. Safari ya maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la Uturuki nchini Libya, upinzani wa jenerali muasi, Khalifa Haftar dhidi ya safari hiyo na sisitizo lake la kushambuliwa wanajeshi wa Uturuki, vilevile masharti yake kwa ajili ya kuondoka Libya wanajeshi hao, vimeendeleza mgogoro wa ndani wa Libya licha ya mazungumzo yanayofanyika sasa baina ya makundi hasimu.

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Libya, Stephanie Williams amesema kuwa kwa sasa zaidi ya wanajeshi na mamluki elfu 20 wa kigeni wako nchini Libya na ametahadharisha kuhusu uwezekano wa kusambaratika makubaliano ya kusitisha vita yaliyotiwa saini tarehe 23 Oktoba mwaka jana mjini Geneva. 

Stephanie Williams

Katika upande wa ndani, makundi ya kisiasa ya Libya yanaendelea kuzozana, suala ambalo linazorotesha mwenendo wa mazungumzo ya amani. Wakati huo huo wataalamu wa mambo wanasisitiza kuwa ili kuweza kupatikana mapatano madhubuti kuhusu mgogoro wa Libya kuna udharura wa kushirikishwa makundi yote ya kisiasa ya nchi hiyo wakiwemo wafuasi wa dikteta wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi. Katika mkondo huo mjumbe wa UN katika masuala ya Libya, Stephanie Williams amesema kuwa kumeundwa kamati ya ushauri kwa ajili ya kikao cha mazungumzo ya kisiasa ambayo wanachama wake wameteuliwa kutoka maeneo mbalimbali ya Libya na wana mielekeo tofauti ya kisiasa. Williams amesema kazi kuu ya kamati hiyo ni kujadili masuala tata ya kuunda serikali moja na kwamba mapendekezo ya kamati hiyo yatawasilishwa katika kikao cha mazungumzo ya kisiasa cha makundi ya kisiasa ya Libya.
Zahr al Taud ambaye ni mtaalamu wa masuala ya siasa anasema: Mgogoro wa Libya hauwezi kutatuliwa bila ya maafikiano yanayodhamini na kulinda mlingano wa kisiasa. Hivyo mazungumzo ya kisiasa baina ya makundi yote ndiyo njia bora zaidi ya kutatua mgogoro wa Libya.
Pamoja na hayo yote Libya imeendelea kuwa uwanja wa mchuano kati ya nchi mbalimbali zinazowania utajiri na maliasili za nchi hiyo. Sambamba na hayo, maambukizi ya virusi vya corona, kuongezeka harakati za makundi ya kigaidi na hatari ya kupanuka zaidi harakati za makundi hayo huko Afrika na Ulaya vimezidisha hatari ya kushadidi mapigano na machafuko ya ndani nchini Libya. 

Hata hivyo kufanyika uchaguzi wa mabaraza ya miji nchini Libya katika mazingira ya sasa kunatambuliwa kuwa ni tukio zuri na chanya na kielelezo cha irada na azma ya makundi mengi ya kisiasa na wananchi wa Libya kwa ujumla kwa ajili ya kuijenga upya nchi hiyo na kuanza kipindi kipya katika nchi hiyo iliyoharibiwa na vita.    

Tags