Jan 15, 2021 14:51 UTC
  • Bobi Wine ajitangaza mshindi wa uchaguzi wa rais Uganda; Museveni aongoza

Licha ya matokeo ya awali ya uchaguzi wa rais nchini Uganda kuonesha kuwa Rais Yoweri Museveni yupo kifua mbele, lakini mgombea mkuu wa upinzani, Bobi Wine tayari ameshajitangaza kuwa mshindi wa uchaguzi huo uliofanyika jana Alkhamisi.

Wine ambaye amegombea kiti hicho kupitia chama cha NUP amewaambia waandishi wa habari jijini Kampala kuwa, "tumeibuka na ushindi wa kishindo, nina imani kubwa kuwa tumembwaga dikteta kwa kura nyingi sana."

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 38 na ambaye jina lake la asili ni Robert Kyagulanyi Ssentamu, ameyataja matokeo ya muda yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi yanayoonesha kuwa Rais Museveni anaongoza kuwa 'dhihaka'.

Amesema, "Wananchi wa Uganda wamepiga kura kwa wingi ili kuleta mageuzi katika uongozi, kutoka utawala wa kidikteta hadi serikali ya kidemokrasia."

Muda mfupi baada ya kujitangaza mshindi wa urais, wanajeshi wa nchi hiyo wameripotiwa kuvamia na kuyazingira makazi yake mwanasiasa huyo. Hata hivyo Deo Akiki, Naibu Msemaji wa Jeshi la Uganda amekanusha madai hayo akisisitiza kuwa, waliovamia nyumba ya Bobi Wine ni raia na wala si maafisa usalama.

Kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi, Rais Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 76 na ambaye ameiongoza Uganda kwa miaka 35, anaongoza kwa asilimia 63 akifuatiwa na Wine mwenye asilimia 28. 

Baadhi ya wagombea wa upinzani wameripotiwa wakisema kuwa, uchaguzi wa jana ulitawaliwa na dosari nyingi hivyo hawako tayari kuyakubali matokeo ya uchaguzi huo.

Wine (kulia) na Rais Museveni mwenye miaka 76

Serikali ya Rais Museveni ambayo ilifunga mtandao wa intaneti saa chache kabla upigaji kura kuanza katika kile ambacho kilitajwa kuwa ni hatua ya kudumisha usalama, imepuuzilia mbali madai hayo ya Wine.

Msemaji wa serikali, Ofwono Opondo ameiambia kanali ya al-Jazeera ya Qatar kuwa, "Tulitaraji haya tokea mwanzo. Hata kabla ya uchaguzi, (Wine) aidai kuwa matokeo yatachakachuliwa. Hamna jipya, madai ya namna hiyo tumeshayazoea katika chaguzi za hapa Uganda."

 

 

Tags