Jan 17, 2021 02:21 UTC
  • Sudan yamshukuru Salva Kiir kwa kujitolea kuipatanisha na Ethiopia

Waziri Mkuu wa Sudan amemshukuru Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini kwa kujitolea kuwa mpatanishi kati ya nchi yake na Ethiopia.

Abdullah Hamdok ametoa shukrani hizo wakati alipoonana na mjumbe maalumu wa Salva Kiir na kusema kuwa, ubunifu huo wa Rais Salva Kiir wa kujitolea kuzipatanisha Sudan na Ethiopia ni jambo la kupigiwa mfano.

Vile vile amesema, hatua hiyo ya Rais Salva Kiir ni kuzidi kuonesha kuwa njia pekee ya kutatua migogoro ya Afrika ni mazungumzo. Vile vile amemshukuru rais huyo wa Sudan Kusini kwa juhudi zake za kupigania utulivu na usalama kwenye eneo hilo.

Hadi tunapokea habari hii, viongozi wa Ethiopia hawakuwa wametoa majibu wala kuonesha hisia zozote kuhusu kujitolea huko Rais Kiir kuzipatanisha Addis Ababa na Khartoum.

Mkoa wa al Qadarif nchini Sudan

 

Ugomvi katika eneo la mapakani baina ya Sudan na Ethiopia umekuwa mkubwa tangu mwanzoni mwa mwezi Novemba 2020 wakati Ethiopia ilipoendesha operesheni za kijeshi za kuwang'oa waasi wa eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia. Vita hivyo vimepelekea zaidi ya wakimbizi 50 elfu wa Ethiopia wakimbilie mashariki mwa Sudan.

Ugomvi mkubwa uliopo baina ya Addis Ababa na Khartoum ni mashamba ya kilimo katika eneo la al Fushqa mkoani Qadarif kwenye mpaka wa Sudan na Ethiopia. 

Juzi Ijumaa kuliripotiwa habari kwamba, Sudan imeanza kutekeleza sheria ya kuzuia ndege kupaa kwa masafa ya chini ya futi 29,000 katika anga ya Qadarif la mpakani na Ethiopia. Uamuzi huo ulichukuliwa baada ya ndege za kivita za Ethiopia kuingia bila ya ruhusa katika anga ya Sudan.

Tags