Jan 17, 2021 08:02 UTC
  • Watu wengine 32 wauawa katika mapigano ya kikabila Darfur, Sudan

Watu wasiopungua 32 wameuawa huku wengine wengi wakijeruhiwa katika mapigano ya kikabila baina ya Waarabu na wasiokuwa Waarabu katika mkoa wa Darfur Magharibi nchini Sudan.

Salah Saleh, daktari na mkurugenzi wa zamani wa Hospitali Kuu ya Genena, makao makuu ya mkoa huo amesema mbali na 32 kuuawa, wengine karibu 80 wamejeruhiwa katika mapigano hayo.

Mapigano hayo ya kikabila yameripotiwa kuanza Ijumaa ya juzi baada ya Muarabu kuuawa kwa kuchomwa kisu katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Krinding katika mji huo.

Haya yanajiri chini ya wiki tatu baada ya Kikosi cha pamoja cha kusimamia amani cha Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika katika jimbo la Darfur la magharibi mwa Sudan UNAMID kutangaza kuwa kimekamilisha shughuli zake katika jimbo hilo zilizodumu kwa muda wa miaka 13. Mashirika na asasi mbalimbali za kibinadamu zimekuwa zikitahadharisha kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu katika jimbo hilo.

Eneo la Darfur mwaka 2003 lilikumbwa na mapigano ya umwagaji damu kati ya serikali ya wakati huo ya Sudan chini ya uongozi wa Rais aliyeenguliwa mdarakani, Omar al-Bashir, na wapinzani wa serikali. Karibu wakazi 300,000 wa jimbo hilo waliuawa katika mapigano hayo.

Ramani inayoonesha mkoa wa Darfur wa magharibi mwa Sudan

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Baraza la Uongozi wa Sudan amesema nchi hiyo haitaki kuingia katika vita na jirani yake Ethiopia. Abdulfattah al-Burhan alisema hayo jana Jumamosi na kuongeza kuwa, ameafikiana na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed juu ya kutumwa askari wa Sudan katika mpaka wa nchi mbili hizo. Nchi mbili hizo jirani zimekuwa na tofauti za mipaka za miaka mingi na hadi sasa hazihafanikiwa kuzitatua.

Ugomvi katika eneo la mapakani baina ya Sudan na Ethiopia umekuwa mkubwa tangu mwanzoni mwa mwezi Novemba 2020 wakati Ethiopia ilipoendesha operesheni za kijeshi za kuwang'oa waasi wa eneo la Tigray la kaskazini mwa Ethiopia. Vita hivyo vimepelekea zaidi ya wakimbizi 50 elfu wa Ethiopia wakimbilie mashariki mwa Sudan.

Tags