Jan 18, 2021 10:50 UTC

Wananchi wa Sudan wameandamana mjini Khartoum, kupinga uamuzi wa nchi yao kuanzisha uhusiano na utawala haramu wa Israel.

Kwa mujibu wa taarifa wananchi waliokuwa na hasira waliandamana mbele ya jengo la Baraza la Mawaziri mjini Khartoum siku ya Jumapili. 

Washiriki wa maandamano hayo walikuwa wamebaba mabango yenye maandishi ya kupinga uhusiano baina ya Sudan na utawala wa Israel.

Waandamanaji pia wametoa nara dhidi ya Marekani na serikali ya mpito ya Sudan huku wakitoa tishio la kuandaa maandamano dhidi ya serikali katika majimbo yote ya Sudan.

Katika mjumuiko huo waandamanaji waliteketeza moto bendera ya utawala haramu wa Israel huku wakisistiza kuwa utawala wa Israel unakalia ardhi za Palestina kwa mabavu mbali na kuwaangamiza kwa umati Wapalestina.

Wasudan waandamana kupinga uhusiano wa nchi yao na Israel

Mwaka wa 2020, nchi nne za Kiarabu ambazo ni Umoja wa Falme za Kiarabu, Bahrain, Sudan na Morocco zilitangaza kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel na hivyo kujiunga na Misri na Jordan ambazo zinautambua rasmi utawala huo ghasibu.

Inaaminika kuwa Saudi Arabia nayo tayari ina uhusiano wa siri na utawala haramu wa Israel lakini inahofia kuutangaza uhusiano huo hadharani utaharibu kabisa sura yake katika ulimwengu wa Kiislamu.

Hatua ya nchi hizo kuanzisha uhusiano na Israel imetajwa kuwa ni usaliti kwa harakati za kupigania ukombozi wa Palestina.

 

Tags